Aug 01, 2021 02:30 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Tuna wasiwasi baada ya misaada ya kibinadamu kuchelewa kufika Tigray Ethiopia

Umoja wa Mataifa Uujmetangaza kuwa, una wasiwasi kufuatia ucheleweshaji katika kupeleka misaada ya kibinadamu jimboni Tigray, kwa minajili ya kukabiliana na hali mbaya inayolikumba jimbo hilo la kaskazini mwa Ethiopia.

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA Jens Laerke, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kuwa, usafirishaji na upelekaji wa misaada ya kibinadamu katika jimbo hilo ndio changamoto kubwa kwa sasa.

Taarifa ya mashirika ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, yanakabiliwa na changamoto ya kusafirisha misaada vikiwemo vifaa na wafanyakazi katika eneo hilo na kuwa zaidi ya dola milioni 430 zinahitajika ili kukidhi mahitaji huko Tigray hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) 

 

Aidha Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema kuwa, baada ya miezi minane ya ghasia na machafuko katika jimbo la Tigray, watu milioni 5.2 ambao ni karibu asilimia 90 ya idadi ya watu wote wa jimbo hilo wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Katika upande mwingine, baadhi ya mashirika ya misaada ya kibinadamu yametahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea maafa ya kibinadamu endapo misaada hiyo haitawafikia walengwa kwa wakati.

Mapigano kati ya serikali jeshi la ya Ethiopia na waasi wa harakati ya TPLF yalianza mwezi Novemba mwaka jana. Hadi sasa mapigano hayo yamewalazimisha watu karibu milioni mbili kuwa wakimbzi na wengine laki nne kukabiliwa na hali ngumu na ukosefu wa chakula. 

Tags