Aug 01, 2021 02:31 UTC
  • Nchi 14 za Kiafrika zaafikiana kuutimua utawala haramu wa Israel katika Umoja wa Afrika

Algeria imetangaza kuwa, imeafikiana na nchi nyingine 13 kwa ajili ya kuanzisha kampeni ya kuutimua utawala haramu wa Israel katika Umoja wa Afrika baada ya utawala huo ghasibu kuteuliwa hivi karibuni kuwa mwanachama mtazamaji katika umoja huo.

Kanali ya Televisheni ya al-Waqi ya Algeria imetangaza kuwa, nchi hiyo imeanzisha kampeni maalumu ya kuunda kundi la nchi zitakazokataa Israel kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika na kwamba, lengo la hatua hiyo ni kulinda misingi ya Umoja wa Afrika katika kuliunga mkono taifa la Palesrtina.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, tayari nchi za Afrika Kusini, Tanzania, Tunisia, Eritrea, Senegal, Niger, Comoro, Gabon, Nigeria, Zimbabwe, Liberia na visiwa vya Ushelisheli vimetangaza kuunga mkono uamuzi huo wa Algeria. Aidha Namibia na Algeria tayari zilishatangaza pia kulaani hatua ya Umoja wa Afrika ya Kuupasisha utawala haramu wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji wa umoja huo.

Ramtane Lamamra Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria

 

Ramtane Lamamra Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria amesisitiza kuwa, uamuzi huo uliechukuliwa pasi na kuweko mashauriano ya hapo kabla baina ya nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika.

Kabla ya Algeria, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) pia imekosoa vikali hatua ya Umoja wa Afrika (AU) ya kuupa utawala wa Kizayuni wa Israel kibali cha kuwa mwanachama mtazamaji wa umoja huo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, upinzani dhidi ya utawala haramu wa Israel umeendelea kuongezeka ambapo utawala huwa umepata pigo katika mashindano yanayoendelea ya Olimpiki ya Tokyo 2020 baada ya wanamichezo kutoka Algeria na Sudan kukataa kupambana na washindani wao kutoka Israel.