Aug 02, 2021 10:22 UTC
  • Matukio ya Tunisia, ajenda kuu ya mazungumzo ya waziri wa mambo ya nje wa Algeria Misri

Ramtane Lamamra, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria ambaye yuko Misri amekutana na kuzungumza na rais wa nchi hyo kuhusu uhusiano wa nchi mbili na matukio ya Tunisia.

Katika mazungumzo hayo pande mbili zimejadili matukio yanayoendelea katika nchi jirani ya Tunisia na kutangaza uungaji mkono wao kwa Rais Kais Saied wa nchi hiyo pamoja na juhudi zote zinazofanyika kwa ajili ya  kulinda usalama na uthabiti wa kisiasa wa nchi hiyo.

Pande mbili pia zimejadili na kubadilishana mawazo juu ya namna ya kuimarisha uhusiano wa nchi mbili hasa katika nyanja za biashara, uchumi, kuongeza viwango vya uwekezaji, uratibu wa kisiasa na kiusalama na kubadilishana hahari zinazohusiana na mapambano dhidi ya ugaidi na mielekeo ya kupindukia mipaka katika eneo.

Abdulfattah as-Sisi

Katika mazungumzo yao, Waziri Ramtane Lamamra na Rais Abdulfattah as-Sisi wa Misri wamejadili pia baadhi ya mambo ya kieneo yenye umuhimu kwa nchi mbili na hasa suala la Libya na kusisitiza juu ya kutekelezwa maazimio ya kimataifa na ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala zima la kuandaliwa uchaguzi mkuu na kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo askari na mamluki wote wa kigeni.

Kuhusu Bwawa la an-Nahdha linalojengwa katika Mto Nile nchini Ethiopia, Rais as-Sisi amesema kuwa nchi yake bado inashikilia msimamo wake wa awali wa kutetea haki zake za kihistoria kuhusu maji ya mto huo. Amezitaka pande zote husika kuketi kwenye meza ya mazungumzo zikiwa na nia nzuri na irada thabiti ya kisiasa kwa lengo la kufikiwa mapatano mapana yatakayotekelezwa kwa maslahi ya pande zote na hivyo kufikiwa utatuzi wa mwisho kuhusu bwawa hilo.

Tags