Aug 02, 2021 11:04 UTC
  • Majenerali wa kijeshi Madagascar waswekwa ndani kwa 'kutaka kumuua Rais'

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Madagascar ametangaza habari ya kutiwa mbaroni majenerali watano wa jeshi na maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa polisi ya nchi hiyo wakituhumiwa kuhusika na njama iliyofeli ya kutaka kumuua Rais wa nchi hiyo, Andry Rajoelina.

Berthine Razafiarivony alisema hayo jana Jumapili katika kikao na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, "kufikia sasa watu 21 wamekamatwa na wanachunguzwa, wakiwemo raia wawili wa Ufaransa."

Amesema watu wanne miongoni mwa waliokamatwa ni maafisa waliostaafu wa polisi na kijeshi wa ndani na nje ya nchi hiyo ya kusini mashariki mwa bara Afrika.

Ameongeza kuwa, raia watano ni miongoni mwa washukiwa hao waliotiwa mbaroni, wakituhumiwa kuhusika na jaribio lililofeli la kutaka kumuua rais wa nchi hiyo mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Madagascar, vyombo vya usalama vimenasa pia magari mawili, bunduki na dola 250,000 zilizokuwa mikononi mwa washukiwa hao.

Rais Rajoelina wa Madagascar

Andry Rajoelina, mwenye umri wa miaka 47, ni maarufu sana miongoni mwa wawanchi wa Madagascar kwani aliwahi kuwa meya wa mji mkuu Antananarivo mwaka 2007, kabla ya kutwaa madaraka ya nchi kwa kusaidiwa na jeshi la nchi hiyo,  ambapo aliongoza kwa miaka mitano, kuanzia 2009 hadi 2013.

Rajoelina alirejea tena katika uga wa siasa nchini Madagascar baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi wa urais wa Disemba mwaka 2018, baada ya kumbwaga mpinzani wake mkuu Marc Ravalomanana.

 

 

 

Tags