Aug 03, 2021 06:20 UTC
  • Ghannouchi akosoa uingiliaji wa nchi za kigeni katika mambo ya ndani ya Tunisia

Rached Ghannouchi Spika wa Bunge lililosimamishwa la Tunisia amekosoa uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Ghannouchi ameashiria himaya ya Imarati kwa maamuzi yaliyochukuliwa na Rais Kais Saeid wa Tunisia ya kumfukuza kazi Waziri Mkuu, kusitisha shughuli za Bunge na kushika madaraka yote ya nchi na kusema: Imarati inavitambua vyama vya Kiislamu kuwa ni tishio kwa mipango yake ya kupanua ushawishi na satua yake na imechukua uamuzi wa kuzima mapinduzi ya Kiarabu katika nchi yalipoanzia yaani Tunisia. 

Mgogoro wa kisiasa umepamba moto zaidi nchini Tunisia katika siki za hivi karibuni. Kufuatia malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali na chama cha Ennahdha ambacho ndicho chenye viti vingi zaidi katika Bunge la Tunisia, Rais Kais Saeid alimfuta kazi Waziri Mkuu Hichem Mechichi na kusitisaah shughuli za Bunge la nchi hiyo. Vilevile amefuta kinga ya kisheria ya wabunge na kushikilia madaraka yote ya Tunisia. Hatua hiyo ya Kais Saeid imetambuliwa na vyama vya upinzani kuwa ni mapinduzi baridi na kwamba amerejesha nchini humo utawala wa kidikteta. Rais wa Tunisia amekanusha madai hayo akisema yeye si dikteta na kwamba amechukua hatua hiyo kulinda mamlaka ya nchi hiyo. 

Sambamba na hayo Spika wa Bunge lililosimamishwa la Tunisia, Rached Ghannouchi amefichua kwamba, nchi za kigeni zinaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Vilevile Naibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Ennahdha, Ali al-Aridh, ametangaza kuwa, maamuzi yaliyotangazwa na Rais Kais Saied ni mapinduzi dhidi ya asasi za serikali, Katiba na mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo. 

Kais Saied

Katika miaka ya hivi karibuni nchi nyingi za Kiarabu ikiwemo Misri, Libya na Tuisia zimekumbwa na mageuzi na mabadiliko makubwa kutokana na malalamiko na maandamano ya wananchi wanaopinga hali mbaya ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi hizo. Hata hivyo mabadiliko hayo hayajazaa matunda kutokana na uingiliaji wa madola ya kigeni na kinyume chake, yamezidisha migogoro ya kisiasa na ukosefu wa amani katika nchi hizo. Katika uwanja huu nchi kama Imarati na Saudi Arabia zimekuwa zikitumia utajiri wa mafuta kwa ajili ya kuvuruga usalama na kudumisha machafuko katika baadhi ya nchi za Kiarabu za Magharibi mwa Asia ili kwa njia hiyo kuficha kufeli kwa watawala wa nchi hizo na kwa upande mwingine kupanua ushawishi na satua zao  katika Ulimwengu wa Kiarabu. Ukweli huo ulionekana waziwazi huko Libya, Yemen, Misri. Nchi hizo za Kiarabu yaani Saudia na Imarati, kwa upande mmoja haziridhii kuona ustawi wa nchi nyingine za Kiarabu na kwa upande mwingine zinatumia utajiri wao wa mafuta kuimarisha satua na uchawishi wa kisaisa na kiuchumi katika nchi nyingine. Harakati hii ya baadhi ya nci za Kiarabu pia inaungwa mkono na madola ya Magharibi kama Ufaransa na Marekani.

Mujtahid ambaye ni mchambuzi na mfichuaji maarufu wa siri za utawala wa kifalme wa Saudia anasema: “Ufaransa ikishirikiana na Saudi Arabia, Imarati na Misri zilipanga mapinduzi baridi ya Tunisia, na yanayojiri katika nchi hiyo ni njama inayotekelezwa na Rais Kais Saeid kwa ajili ya kuangamiza haraki ya mapinduzi ya wananchi kama ilivyofanyika nchini Misri wakati jenerali Abdel Fattah al Sisi alipotumiwa kuvuruga matunda ya mapinduzi ya wananchi dhidi ya dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Hosni Mubarak.”

Mfalme Salman wa Saudia na kiongozi wa Misri, Abdel Fattah al Sisi

Ni kwa sababu hii ndiyo maana wananchi wa Tunisia wanasisitiza udharura wa kulindwa malengo ya mapinduzi yao dhidi ya utawala wa kidikteta na kutilia mkazo kwamba, kamwe hawatatoa fursa kwa madola ya kigeni na vibaraka wao kuendelea kuvuruga usalama na hali na ndani ya nchi yao.  

Tags