Aug 04, 2021 00:54 UTC
  • Tuhuma mpya za Mwendesha Mashtaka dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky

Mwendesha Mashataka wa Jimbo la Kaduna nchini Nigeria ametoa tuhuma mpya dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ikiwa ni siku chache tu baada ya kutolewa hukumu ya kuachiliwa huru kiongozi huyo.

Jumatano iliyopita Mahakama ya Kaduna ilitoa hukumu ya kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat baada ya kushikiliwa mahabusu kwa kipindi cha takribani miaka 6 iliyoambatana na masaibu na mateso mengi. Kwa mujibu wa hukumu hiyo, wawili hao walifutiwa tuhuma zote nane walizokuwa wakikabiliwa nazo kama kuvuruga nidhamu ya umma na kufanya mikusanyiko iliyo kinyume cha sheria.

Filihahi inaonekana kumeibuka senario mpya dhidi ya Sheikh Zakzaky ambapo Dari Bayero, Mwendesha Mashtaka wa Jimbo la Kaduna ametangaza kuwa, kumetolewa tuhuma nyingine katika mahakama nyingine dhidi ya Sheikh Zakzaky siku mbili tu baada ya kuachiliwa huru kwake. Tuhuma hizo mpya zinajumuisha ugaidi na usaliti dhidi ya taifa. Mwendesha Mashtaka huyu amedai kuwa, wakati wa kushikiliwa kwake Sheikh Zakzaky alikataa kupokea agizo jipya la Mwendesha Mashtaka kuhusiana na tuhuma dhidi yake.  Kwa sasa Mahakama Kuu ya Federali ya Kaduna imesimamisha shughuli zake kwa ajili ya likizo na kwamba, mwendesha mashataka atalifungua tena faili la Sheikh Zakzaky mwezi ujao wa Septemba.

Inaonekana kuwa, lengo kuu la tuhuma mpya dhidi ya Sheikh Zakzaky ni kumtia wahaka na wakati huo huo kumzuia asirejee nchini Nigeria. Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, Shekh Zakzaky akiwa na lengo la kupata matibabu aliondoka nchini humo siku moja tu baada ya kuachiliwa huru. Wataalamu wa masuala ya kitiba wamesisitiza kuwa, matibabu ya kitaalamu anayohitajia Sheikh Zakzaky yanapatikana tu nje ya nchi.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat

 

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mke wake walikamatwa Desemba 13, 2015 katika hujuma na shambulio lililofanywa na askari wa jeshi la serikali dhidi ya Husainiya iliyoko katika mji wa Zaria.

Siku hiyo aliyokamatwa Sheikh Zakzaky, vikosi vya jeshi la Nigeria viliwafyatulia risasi Waislamu waliokuwa wamekusanyika kwenye Husaniya hiyo na nyumba yake na kuwaua shahidi mamia kadhaa miongoni mwao, wakiwemo watoto watatu wa kiume wa kiongozi huyo wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Sheikh Zakzaky alijeruhiwa vibaya katika ukandamizaji huo wa jeshi la Nigeria ambao ulimpelekea kupoteza jicho lake moja na kudhoofisha pakubwa la pili.Mbali na ukandamizi huo, Sheikh Zakzaky na mkewe waliendelea kupata mateso mengi wakiwa kizuizini ambapo walinyimwa hata huduma ya msingi kabisa ya matibabu. Katika kipindi hicho chote serikali ya Nigeria ilitumia kila mbinu kumlazimisha Sheikh Zakkzaky akubali tuhuma alizobambikiziwa lakini licha ya mateso hayo yote, mwanamapambano huyo aliendelea kusimama imara na kushikilia misimamo yake ya kidini na kutotetereka hata kidogo.

Pamoja na hayo tuhuma mpya za Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kaduna ni ishara ya wazi kwamba, serikali ya Nigeria ambayo mwka 2019 iliitangaza Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kuwa ni kikundi haramu na kupiga marufuku shughuli zake, filihahi inataka kupitia njia ya kutoa tuhuma mpya kwa mara nyingine tena imtie mbaroni Sheikh Zakzaky na kumpandisha kizimbani, na kwa utaratibu huo izuie hatua zozote za kutaka kuanzishwa tena shughuli za harakati hiyo nchini Nigeria.

Sheikh Zakzaky alijeruhiwa vibaya Disemba 2015 wakati jeshi la Nigeria liliposhambulia nyumbani kwake

 

Katika upande mwingine, hatupasi kusahau mashinikizo mtawalia kutoka nje yanayofanywa na Marekani, utawala vamizi wa Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel dhidi ya serikali ya Abuja ili kuzuia harakari za Waislamu wa Kishia nchini Nigeria zinazoongozwa na Sheikh Zakzaky hasa kwa kutolewa tuhuma mpya dhidi ya mwanazuoni huyo. Utawala wa Saudia ukiwa muenezaji wa mafundisho potovu ya Kiuwahabi na adui wa wazi wa Mashia, umekuwa ukitumia mbinu mbalimbali ili kuzuia kuenea Ushia nchini Nigeria.

Abayomi Azikiwe mwanaharakati na mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: Saudi Arabia ina ushawishi mkubwa kwa serikali ya Nigeria na hata hujuma na mashambulio dhidi ya Sheikh Zakzaky na mauaji ya maelfu ya wafuasi wake yamefanyika kwa amri na maagizo ya utawala wa Aal Saud. Wakati huo huo, utawala haramu wa Israel nao ukiwa na lengo la kupanua satwa na upenyaji wake barani Afrika, unaona kuwa, kuenea Ushia nchini Nigeria ambayo ina idadi kubwa ya watu katika bara hilo kunakinzana kikamilifu na malengo yake.

Katika kipindi cha kushikiliwa kwa muda mrefu Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe, tawala vamizi za Saudia na Israel zilifanya kila ziwezalo ili kuandaa mazingira ya kuhukumiwa kiongozi huyo wa Kiislamu. Pamoja na hayo, kufutiwa mashtaka Sheikh Zakzaky na kisha kuachiliwa huru na kuweko uwezekano wa kuanza tena harakati za Kiislamu za kundi hilo katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kumepelekea kupikwa tena njama na serikali ya Nigeria ikishirikiana na Wazayuni na Aal Saud ili kutiwa mbaroni na kushikiliwa tena kizuizini Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Tags