Aug 04, 2021 07:34 UTC
  • Roboti wapima Covid-19 na kunyunyiza dawa katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, Kenya

Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP nchini Kenya linaendesha programu ya majaribio ya kutumia roboti katika kupima afya za wasafiri wanaoingia na kutoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa Jomo wa Kenyatta jijini Nairobi pamoja na Hospitali Kuu ya Taifa ya Kenyatta lengo likiwa ni kuongeza ufanisi na kuwapunguzia mzigo watendaji wa sekta ya afya.

Video ya Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP inaonesha roboti watatu wakiwa wamefungwa vifaa viwili vinavyomwaga dawa ya kuua vijidudu, kupima  joto la mwili, kufuatilia, kutunza taarifa za abiria pamoja na usimamizi wa wagonjwa. 

Mwakilishi mkazi wa UNDP nchini Kenya Walid Badawi anasema majina ya roboti hao watatu ni  Jasiri, Tumaini na Shujaa.  

“Mwanzoni mwa janga hili la Corona UNDP tulitoa fursa ya kusaidia ulimwengu kulingana na maono yetu kama shirika la maendeleo katika maeneo ya kujiandaa, kukabiliana na kupona changamoto zilizoletwa na janga hili”, amesema Bwana Badawi. 

Wasafiri wakipimwa joto la mwili katika uwanja wa ndege

Watendaji kadhaaa katika uwanja huo na halikadhalika Hospitali Kuu ya Kenyatta jijini Nairobi wamepatiwa mafunzo ambapo Dkt Amina Guleid ni mwenyekiti wa kamati ya kusimamia programu hii ya roboti na  anasema, “mpaka sasa tumeshawafundisha wataalamu wetu watano wa TEHAMA namna ya uendeshaji wa roboti hawa, na tunaendelea na watoa huduma wengine wa afya, na madaktari ambao watatoa ushauri wa kitaalamu kwenye masuala ya kliniki. Lakini pia tunaye mtaalamu wa afya ambaye anahusika kwenye eneo la kufukiza dawa na ndio anatuongoza namna sahihi ya kufukiza.” 

 Roboti hao pia wanaepusha wahudumu wa afya kuwa karibu na abiria na hivyo kupunguza hatari ya kupata maambukizi ya Corona. 

Utaalamu huo wa kutumia roboti umebuniwa na kampuni ya Zorabots Afrika Limited chini ya ufadhili wa UNDP Rwanda, na Mkurugenzi mtendaji wake Benjamin Kerenzi anasema roboti hao wana uwezo wa kuchakata takwimu na kutoa taarifa wakati huo huo, hivyo kuwasaidia wafanya maamuzi kuwa na taarifa sahihi.../

 

Tags