Aug 04, 2021 07:54 UTC
  • Nchi saba za Kiarabu Afrika zalalamikia AU kuipa Israel hadhi ya mwanachama mtazamaji

Nchi saba za Kiarabu wanachama wa Umoja wa Afrika AU zimelalamikia rasmi uamuzi wa upande mmoja uliochukuliwa na mkuu wa kamisheni ya umoja huo ya kuupatia utawala haramu wa Kizayuni wa Israel hadhi ya kuwa "mwanachama mtazamaji" katika taasisi hiyo kuu ya bara la Afrika.

Balozi za nchi hizo saba ambazo ni Mauritania, Misri, Algeria, Tunisia, Libya, Visiwa vya Komoro na Djibouti leo zimetuma barua rasmi kulalamikia uamuzi uliochukuliwa na mkuu wa kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki wa kuupatia utawala wa Kizayuni hadhi ya kuwa "mwanachama mtazamaji" wa umoja huo na kupokea hati ya utambulisho ya balozi wa utawala huo ghasibu.

Mkuu wa kamisheni ya AU, Moussa Faki

Sehemu moja ya barua hiyo imeeleza kwamba, kwa kuzingatia msimamo thabiti wa kuunga mkono kadhia ya Palestina na kulaani hatua zote zinazochukuliwa na Israel dhidi ya haki za taifa rafiki na ndugu la Palestina, uamuzi huo unagongana na maslahi matukufu ya Umoja wa Afrika, thamani, vigezo na taratibu unazofuata umoja huo.

Nchi hizo aidha zimetangaza kuwa, uamuzi wa Moussa Faki ni kosa lisilokubalika la kiutendaji na kisiasa linalokiuka vigezo vya utoaji hadhi ya uanachama mtazamaji na mfumo wa utoaji itibari wa Umoja wa Afrika ambao ulipitishwa na baraza lake la utendaji Julai 2005.../