Aug 04, 2021 12:18 UTC
  • Amnesty International yaitaka Tanzania itoe ushahidi au imuachie huru Freeman Mbowe

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limesema kuwa, serikali ya Tanzania inapaswa kutoa ushahidi wa kesi dhidi ya kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Tanzania Freeman Mbowe na ikishindwa kufanya hivyo basi iamuachie huru.

Taarifa ya Amnesty inakuja huku Freeman Mbowe akitarajiwa kupandishwa kizimbani mapema kesho siku ya Alkhamisi.

Taarifa ya Amnesty International imesema: ‘’uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umeleta matumaini ya uhuru wa kujieleza, lakini vitendo vya hivi karibuni vya kukamatwa kwa wanachama wa vyama vya upinzani vinatia wasiwasi kama uhuru huu utaendelea ama hali itarudi kama ilivyokuwa awali’’.

Polisi nchini Tanzania imesisitiza kuwa Mbowe amefanya makosa na ushahidi upo.

Freeman Mbowe, kiongozi wa chama cha upinzani cha CHADEMA

 

‘’Wafuasi wa CHADEMA wanadhani Mbowe ameonewa na kuwa yeye ni malaika hawezi kufanya makosa, lakini kesi hii iko mahakami hivyo tuachie mahakama ifanye kazi yake na ukweli utajulikana’’ alisema IGP Simon Sirro mkuu wa polisi Tanzania.

Kiongozi huyo wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, alitiwa mbaroni alfajiri ya kuamkia Julai 21 akiwa katika hoteli ya Kingdom mtaa wa Ghana alikokifikia kwa ajili ya kushiriki kongamano la Katiba Mpya lililoandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).

Hata hivyo, siku iliyofuata Msemaji wa Polisi nchini humo, David Misime aliueleza umma kuwa Mbowe anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo za kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi na kuua viongozi wa Serikali.