Aug 05, 2021 02:32 UTC
  • Sudan yaazimia kujiunga na mahakama ya kimataifa ya ICC

Serikali ya Sudan imechukua hatua ya kwanza ya kutaka kujiunga na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Abdalla Hamdok, Waziri Mkuu wa Sudan amesema katika taarifa kuwa, muswada wa sheria ya kutaka Sudan ijiunge na Mkataba wa Roma uliobuni ICC umepasishwa kwa kishindo na Baraza la Mawaziri la nchi hiyo.

Amesema karibuni hivi, mkutano wa pamoja baina ya Baraza la Uongozi la Sudan na Baraza la Mawaziri la nchi hiyo utafanyika kwa lengo la kuupasisha muswada huo kuwa sheria.

Hamdok amesisitiza kuwa, "haki na uwajibakaji ni misingi mikuu na madhubuti ya Sudan mpya inayotii sheria, tunayotaka kuijenga." Hata hivyo Waziri Mkuu huyo wa Sudan hajafafanua iwapo hatua ya nchi hiyo kujiunga na ICC ina maana ya kukabidhiwa mtawala wa zamani wa nchi hiyo, Omar Hassan al-Bashir kwa mahakama ya kimataifa au la. 

Abdalla Hamdok

Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu,  Waziri wa Masuala ya Federali wa Sudan alitangaza kuwa, Khartuom imechukua uamuzi wa kumkabidhi al-Bashir kwa mahakama hiyo.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) yenye makao yake mjini Hague Uholanzi, mwaka 2009 hadi 2010 ilimtuhumu rais huyo wa zamani wa Sudan kuwa ametenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu katika eneo la Darfur.

Hata hivyo al Bashir alikanusha tuhuma hizo na kuitaja mahakama ya ICC kuwa ni chombo cha kisiasa. Kwa sasa anazuiliwa katika gereza lenye ulinzi mkali la Kober jijini Khartoum.

Tags