Aug 08, 2021 07:58 UTC
  • Chama tawala Uganda chakanusha madai ya kutaka kuingilia uchaguzi wa Kenya

Chama tawala nchini Uganda cha National Resistance Movement (NRM) kinachoongozwa na Rais Yoweri Museveni kimekishutumu vikali chama kikuu cha upinzani nchini Kenya ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, kwa kudai kuwa kinalenga kushirikiana na Naibu Rais William Ruto kuibua machafuko ya uchaguzi nchini humo.

Gazeti la Taifa Leo la Kenya limemnukuu Katibu Mkuu wa NRM, Richard Todwong akisema kuwa, Rais Museveni hana nia ya kuingilia uchaguzi wa Kenya kumwezesha Dkt Ruto kuibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao 2022.

Kupitia barua yake, Todwong ameonekana kujibu mapigo, baada ya wabunge wa ODM kutoa taarifa ya kukashifu NRM. Todwong katika barua hiyo ameukosoa uongozi wa ODM kwa kuichafua NRM na vile vile kumkosea heshima Rais Museveni.

Sehemu moja ya barua hiyo ya Katibu Mkuu wa NRM inasema, "Matamshi hayo labda yalitokana na tofauti zenu za kisiasa nchini Kenya. Tunaamini kuwa kauli yenu sio msimamo wa chama cha ODM.”

Jumatatu iliyopita, Naibu wa Rais wa Kenya, William Ruto alizuiliwa kusafiri kuelekea nchini Uganda kutokana na kigezo kwamba hakupata idhini kutoka kwa Rais Kenyatta. Wabunge wa kambi ya kisiasa ya Naibu Rais wa Kenya wamekiri kuwa Dkt Ruto analenga kujumuisha washauri wa siasa wa Rais Museveni katika kikosi chake cha kampeni anapojiandaa kuwania urais 2022.

Mahasimu wawili wa kisiasa wa Kenya, Raila Odinga (kushoto) na William Ruto

William Ruto amekuwa akihitilafiana na Rais Uhuru Kenyatta kwa muda sasa. Tarehe 12 mwezi Februari mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta alimkosoa waziwazi na hadharani Naibu wake na kumtaka ama ashikamane na sera za serikali yake au ang'atuke na ujiuzulu.

Wakati huo huo, Paul Bamutaze, mfanyabiashara maarufu wa Uganda ameishtaki Kenya katika Mahakama ya Uadilifu ya Afrika Mashariki (EACJ) yenye makao yake mjini Arusha Tanzania, kulalamikia kauli ya wabunge hao wa ODM dhidi ya NRM.

 

Tags