Aug 14, 2021 00:00 UTC
  • Mapigano baina ya jeshi la serikali na waasi wa Tigray yapamba moto Ethiopia

Mapigano makali yameripotiwa baina ya vikosi vya jeshi la serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa kundi la waasi wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) katika maeneo ya mpaka wa jimbo hilo na Amhara kaskazini mwa Ethiopia.

Mapigano hayo yamepamba moto baada ya serikali ya Addis Ababa kutoa tangaza la kufuta usitishaji vita katika jimbo hilo.

Sambamba na mapigano hayo, msemaji wa jeshi la serikali ya Ethiopia amekanusha madai ya kundi la TPLF kwamba limeteka maeneo zaidi ya jimbo la Amhara. Amesema jeshi limetoa kipigo kikali kwa waasi wa TPLF na kukomboa maeneo yaliyokuwa yamedhibitiwa na wapiganaji wa kundi hilo.

Wakati huo huo wimbi kubwa la wakimbizi liendelea kuwasili katika mji wa Dessie, ambao ni wa pili kwa ukubwa katika mkoa wa Amhara.

Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya eneo la Tigray Novemba mwaka jana, kwa madai kuwa wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) wamelishambulia jeshi la nchi hiyo na kuwaua askari waliokuwa wamelala na kupora zana zao za kijeshi. Hadi sasa mapigano hayo yameua mamia ya watu, mbali kuwalazimisha wengine karibu milioni mbili kuwa wakimbizi na wengine laki nne kukabiliwa na hali ngumu na ukosefu wa chakula.

Tigray

Pande mbili hizo zinazozozana nchini Ethiopia kwa miezi kadhaa sasa zimekataa katakata upatanishi wa jumuiya za kieneo na kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Tags