Aug 20, 2021 00:05 UTC
  • Algeria: Makundi yenye uhusiano na Morocco na Israel ndiyo yaliyohusika na moto wa misituni

Algeria imeuhusisha moto mbaya uliotokea hivi karibuni nchini humo na makundi mawili ambavyo nmayatambua kuwa ni magenge ya "kigaidi", na kusema kuwa moja ya kati ya makundi hayo liungwa mkono na Morocco na Israeli.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais wa Algeria imesema, polisi wamewakamata watu 22 kwa kuhusika na moto huo na kuongeza kuwa, wahusika wakuu ni kundi la Rashad na lile la MAK, linalopigania uhuru na kujitenga mkoa wa Kabylie wa wanaozungumza lugha ya Amazigh.

Ofisi ya Rais wa Algeria imesema kundi la MAK linapata msaada na himaya kutoka nje ya nchi, haswa Morocco na utawala wa Kizayuni wa Israeli.

Taarifa hiyo imesema: "Vitendo vya uhasama visivyokoma vinavyofanywa na Morocco dhidi ya Algeria vimelazimisha kuangaliwa upya uhusiano kati ya nchi hizo mbili."

Imesema usalama utaimarishwa zaidi katika mpaka wa nchi hiyo na Morocco.

Imeongeza kuwa, vyombo vya usalama vitaendeleza juhudi za kuwakamata wale wote waliohusika na moto huo na vilevile wanachama wa makundi hayo mawili ya kigaidi".

Moto mkubwa wa misituni ulitanda eneo la Kaskazini mwa Afrika mwezi huu lakini umekuwa mkali zaidi nchini Algeria, ambako umesababisha uharibifu mkubwa na vifo vya makumi ya watu katika majimbo kadhaa haswa huko Tizi Ouzou katika mkoa wa Kabylie, mashariki mwa mji mkuu Algiers.

Mwezi uliopita, Algeria ilimwita nyumbani balozi wake huko Rabat baada ya mwanadiplomasia wa Morocco huko New York kutaka watu wa eneo la Kabylie nchini Algeria wawe na haki ya kujitawala.

Tags