Aug 20, 2021 14:28 UTC
  • Polisi Nigeria washambulia waombolezaji katika kumbukumbu ya Ashura

Askari polisi nchini Nigeria jana Alkhamisi waliwashambulia waombolezaji katika kumbukumbu ya Ashura ya Imam Hussein (AS) na kuua na kujeruhi kadhaa miongoni mwao.

Waislamu wa Kishia nchini Nigeria jana waliungana na mamilioni ya wafuasi wengine wa Ahlul-Baiti (as) duniani kote katika kumbukumbu ya mauaji ya mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein AS ambapo majimbo ya kaskazini na kusini mwa nchi hiyo yalihuisha kumbukumbu hiyo.

Hata hivyo kama kawaida, askari usalama nchini Nigeria ambao wamekuwa wakiwakandamiza Waislamu wa Kishia nchini humo waliwashambulia waombolezaji hao wa Ashura na kuua na kujeruhi kadhaa miongoni mwao.

Mashuhudu wanasema, waombololezaji wawili wameuawa shahidi na wengine kadhaa wamejeruhiwa, baada ya kufyatulia risasi hai na mabomu ya kutoa machozi katika jimbo la Sokoto.

Habari zaidi zinasema kuwa, hafla za maombolezo ya Ashura mwaka huu huko Nigeria zimefanyika katika majimbo karibu yote ya kaskazini mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi. Aidha maombolezo ya Imam Hussein AS yamefanyika katika baadhi ya miji ya majimbo ya kusini mwa Nigeria.

Matembezi ya amani ya kuadhimisha Ashura ya Imam Hussein AS huko Nigeria

Hii si mara ya kwanza kwa askari wa Nigeria kuwashambulia waombolezaji wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. 

Mwaka 2015 vyombo vya usalama vya Nigeria viliwashambulia Waislamu katika mji wa Zaria waliokuwa katika maombolezo ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein AS na kuwaua na kuwajeruhi mamia miongoni mwao. Aidha Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pamoja na mkewe walitiwa mbaroni.

Tags