Aug 21, 2021 02:27 UTC
  • Uganda yasimamisha shughuli za asasi 54 zisizo za kiserikali

Serikali ya Uganda imesimamisha shughuli za makumi ya asasi za kirai yakiwemo mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Okello Stephen, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kitaifa ya Kusimamia Asasi Zisizo za Serikali nchini humo amesema serikali ya Kampala imesimamisha mara moja operesheni za asasi 54 za kiraia kwa kukiuka kanuni na sheria za nchi.

Amesema asasi 23 zimesimamishwa kwa kuendesha shughuli zake licha ya kumalizika muda wa leseni zao, kinyume cha vifungu vya 31(1) na 32(1) vya Sheria ya Asasi Zisizo za Serikali (NGO) ya mwaka 2016.

Okello amebainisha kuwa, mashirika 15 yamesimamishwa kwa kukanyaga vipengee vya 39(2) na (3) vya sheria hiyo, kwa kukataa kuikabidhi serikali madaftari ya akaunti zake yaliyofanyiwa uhasibu.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kitaifa ya NGO nchini Uganda ameongeza kuwa, asasi nyingine 16 zimesimamishwa, kwa kuendesha shughuli zake pasi na kusajiliwa wala kupewa idhini na mamlaka husika, hivyo kukiuka vipengee vya 29 (1), 31 (1) na 31 (2) vya Sheria ya Asasi Zisizo za Serikali ya mwaka 2016.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye kwa muda sasa anatuhumiwa kukandamiza upinzani na wakosoaji wake

Baadhi ya asasi hizo zilizofungiwa na serikali ya Uganda ni zile za kutetea haki za binadamu, kupigania usawa na demokrasia na za kushinikiza kufanyika mageuzi katika vyombo vya kuendesha uchaguzi nchini humo.

Miongoni mwa mashirika yaliyosimamishwa ni pamoja na  Chapter Four, Africa Institute for Energy Governance (AFIEGO), Western Ankole Civil Society Forum (WACSOF), Citizens’ Concerns Africa, Elohim Power Transforming Africa na Orone Foundation.

 

Tags