Aug 23, 2021 03:32 UTC
  • AMISOM yakiri askari wa Uganda wameua raia nchini Somalia

Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) limekiri kuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF) wanaofanya kazi chini ya mwavuli wa kikosi hicho wameua raia wasio na hatia kusini mwa Somalia.

Katika taarifa, AMISOM imesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa, wanajeshi wa UPDF hivi karibuni waliwaua raia saba katika operesheni iliyofanyika katika eneo la Golweyn jimboni Lower Shabelle, na wala si wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab kama ilivyodaiwa hapo awali.

AMISOM imesema imetuma timu ya maafisa wake kwenda kuzungumza na wanakijiji palipotokea mauaji hayo ili kuwatuliza na kuwahakikishia kuwa askari wa kikosi hicho cha kikanda watahimizwa kuwa makini ili kuzuia mauaji ya raia wasio na hatia.

Wiki iliyopita, AMISOM ilisititiza kuwa, wanajeshi wa UPDF waliwaua wanachama wa kundi la al-Shabaab baada ya magaidi hao kujaribu kuwazingira walipokuwa wanalinda doria katika eneo hilo.

Hata hivyo mashuhuda na maafisa wa serikali ya Somalia walipuuzilia mbali madai hayo ya AMISOM, na kushikilia kuwa waliouawa katika operesheni hiyo ya hivi karibuni walikuwa raia.

Askari wa kikosi cha AMISOM nchini Somalia

Waziri Mkuu wa Somalia, Mohamed Hussein Roble siku chache zilizopita, alimuita Balozi wa Uganda mjini Mogadishu juu ya mauaji hayo katika jimbo la Lower Shabelle, kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Hivi karibuni, Jeshi la Somalia likishirikiana na askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini humo lilifanikiwa kuukomboa mji wa kistrataji wa Janale ulioko kwenye eneo hilo la Lower Shabelle, kusini mwa Somalia, toka mikononi mwa al-Shabaab.

Tags