Aug 24, 2021 07:55 UTC
  • Ripoti: Raia 450 wameuawa DRC kati ya Januari na Julai 2021

Shirika moja la kiraia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limesema mamia ya raia wameuawa ndani ya miezi saba ya kwanza ya mwaka huu 2021.

Gili Gotabo, Mkuu wa shirika la kijamii la Irumu amesema kwa akali raia 450 wameuawa katika mapigano na makabiliano ya silaha nchini DRC baina ya Januari na Julai mwaka huu.

Gotabo amebainisha kuwa, mauaji hayo yamefanywa na magenge ya wabeba silaha na wapiganaji wa ndani na nje ya nchi, hususan wanachama wa genge la kigaidi la ADF. 

Kwa mujibu wa ripoti ya asasi hiyo ya kiraia, watu 300 wameuawa na wapiganaji wa ADF katika miji ya  Tchabi, Boga na Walese Vonkutu, kusini mwa eneo la Irumu.

Maafisa usalama wakilinda doria katika mkoa wa Ituri

Aidha ripoti hiyo imesema, katika kipindi hicho cha miezi saba ya kwanza ya mwaka huu, raia wasiopungua 150 wakiwemo wanawake wameuawa katika miji ya Andisoma, Mobala, Babelebe na Baboabokoe.

Genge hilo linalotokea Uganda na linalodaiwa kuwa na mfungamano na kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) lilishadidisha mashambulio yake ya umwagaji damu tangu mwanzoni mwa mwaka huu hasa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri.

 

Tags