Aug 25, 2021 12:57 UTC
  • Wakimbizi kutoka Afghanistan waanza kuwasili Uganda

Kundi la kwanza la makumi ya wakimbizi kutoka Afghanistan limewasili nchini Uganda.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda imesema katika taarifa kuwa, kundi la kwanza la wakimbizi 51 kutoka Afghanistan limewasili katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki mapema leo, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wakimbizi hao wamefanyiwa upekuzi wa kiusalama sanjari na vipimo vya lazima vya ugonjwa wa Covid-19.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda imekiri kuwa, kuna baadhi ya raia wa nchi hiyo ya Kiafrika wamekwama nchini Afghanistan, na hilo limetokana na ugumu wa kufika katika Uwanja wa Ndege wa Kabul. Hata hivyo inasisitiza kuwa jitihada zote zinafanyika kuhakikisha kuwa Waganda hao wanarejeshwa nyumbani karibuni.

Wakimbizi wa Kiafghani wakisafirishwa kwa basi kutoka Uwanja wa Ndege wa Entebbe

Hivi karibuni, Esther Anyakun Davinia, Naibu Waziri wa Misaada ya Dharura, Majanga na Wakimbizi wa Uganda alisema Rais Yoweri Museveni ameafiki ombi la Marekani la kuwapokea wakimbizi 2,000 wa Kiafghani.

Davinia alisema Waafghani hao watakuwa nchini Uganda kwa muda wa miezi mitatu kabla ya serikali ya Marekani kuwahamishia kwingineko. Kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya Uganda, gharama zote zitakazotumika kipindi wakimbikizi hao watawa nchini zitalipwa na Marekani.

Tags