Aug 27, 2021 10:31 UTC
  • Antonio Guterres
    Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano na vitendo ya uhasama nchini Ethiopia.

Wito huo wa Antonio Guterres umetolewa huku mapigano katika jimbo la Tigray huko kaskazini mwa Ethiopia vikipamba moto zaidi baada ya makundi kadhaa ya waasi kujiunga na lile la TPLF.

Guterres amezitaka pande zote katika mgogoro wa ndani wa Ethiopia kusitisha uhasama mara moja na bila ya masharti yoyote na kuanza mazungumzo ya usitisha vita wa kudumu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ametilia mkazo udharura wa kuondoka vikosi vya majeshi ya kigeni katika ardhi ya Ethiopia.  

Wito huo wa Antonio Guterres umetolewa huku mapigano na vita vikipamba moto na kupanuka zaidi nchini Ethiopia baada ya makundi mengine kadhaa ya waasi kujiunga na Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF).

Tigray

Wapiganaji wa harakti hiyo wamesonga mbele zaidi na kudhibiti maeneo mengi ya jimbo la Tigray lililoko kaskazini mwa nchi hiyo.

Alkhamisi ya jana Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Ethiopia (EHRC) ilitangaza kuwa watu wasiopungua 210 wameuawa katika ghasia na mapigano ya kikabila yaliyojiri kwa siku kadhaa katika eneo la Oromia, magharibi mwa Ethiopia.

Wakazi wa eneo hilo wameiambia EHRC kuwa, watu zaidi ya 150 wameuawa na wapiganaji wa genge hilo linalodai kupigania ukombozi wa watu wa jamii ya Oromo.

Kundi hilo la OLA linakadiriwa kuwa na wapiganaji wapatao 2,800 kwenye sehemu za magharibi na kusini mwa mkoa wa Oromia. Makundi ya waasi katika eneo hilo yanadai kupigania haki za Waoromo ambao ni asilimia 35 ya watu milioni 110 wa Ethiopia.

Tags