Aug 30, 2021 02:28 UTC
  • Waasi wa Tigray, Ethiopia wakataa upatanishi wa mjumbe wa AU

Wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) wamepinga na kukosoa vikali hatua ya Umoja wa Afrika kumteua aliyekuwa rais wa Nigeria kuwa mpatanishi katika mgogoro unaoshuhudiwa kwa miezi kadhaa sasa katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.

Msemaji wa TPLF, Getachew Reda ameandika katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa Twitter jana Jumapili kuwa: Ni upuuzi kuamini kuwa mpango huu utafanikiwa. Ili kutatua mgogoro, kwa uchache unapaswa kutambua uwepo wa mgogoro wenyewe, achilia mbali kuupatia ufumbuzi.

Gatechew ameutuhumu Umoja wa Afrika kwa upendeleo na kusisitiza kuwa: Kamisheni ya AU ilipaswa kwanza kusitisha uungaji mkono wake kwa wanajeshi wa serikali ya Ethiopia katika vita dhidi ya wapiganaji wa TPLF, kabla ya kuteua mpatanishi.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki Mahamat, alitangaza Ijumaa iliyopita kwamba, Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ameteuliwa kuwa mjumbe wa Umoja wa Afrika katika eneo la Pembe ya Afrika.

Taharuki katika eneo la Tigray

Haya yanajiri katika hali ambayo, Obasanjo anatazamiwa kuelekea katika Pembe ya Afrika katika wiki zijazo, huku Umoja wa Afrika ukiziomba pande zote hasimu kumuunga mkono, ili kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo.

Mapigano baina ya jeshi la taifa la Ethiopia na wapiganaji wa harakati ya TPLF yalianza tokea Novemba mwaka jana, na yanaendelea mpaka sasa licha ya Addis Ababa kutangaza usitishaji vita wa upande mmoja mnamo Juni 28. Hadi sasa mapigano hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu, mbali na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi. 

Tags