Sep 01, 2021 11:16 UTC
  • Majirani wa Libya wamaliza mkutano wao; wasisitiza kutopatiwa silaha mamluki

Kikao cha mataifa jirani na Libya kilichokuwa kikifanyika nchini Algeria kimemalizika huku washiriki wa mkutano huo wakisisitizia ulazima wa kuzuia kupatiwa silaha mamluki na wakati huo huo kukabiliana na hatua za kuzusha mifarakano miongoni mwa Walibya.

Kikao cha siku mbili cha majirani wa Libya kimemalizika nchini Algeria huku zikiwa zimepita siku 40 tangu wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walipowataka viongozi wa Libya kuchukua hatua za lazima za kuitisha uchaguzi mkuu nchini humo.

Kikao cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa mataifa 6 jirani na Libya yaani Misri, Chad, Tunisia, Mali, Sudan na Congo Brazzaville kimesisitiza katika taarifa yake mwishoni mwa mkutano huo hapo jana kwamba, wamekubaliana kutumwa ujumbe maalumu wa kutathmini mwenendo wa kisiasa nchini Libya kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu. Ujumbe huo utakutana na kufanya mazungumzo na vyama na mirengo yote ya kisiasa ya nchi hiyo.

Mamluki wanaopigana vita nchini Sudan

Aidha mawaziri hao wamesisitizia udharura wa kuondoka majeshi yote ya kigeni nchini Libya pamoja na mamluki na kuweko ushiriki wa mataifa jirani katika mchakato wa kuikarabati upya nchi hiyo iliyoharibiwa vibaya na vita.

Algeria imekuwa mwenyeji wa mkutano wa Libya kwa mara ya pili mtawalia na hivyo kuongoza juhudi za kieneo na kimataifa za kupatiwa ufumbuzi matatizo ya nchi hiyo.

Wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, uwepo wa makundi ya kigaidi amilifu nchini Libya bado lingali ni tatizo kuu na la kimsingi kwa nchi hiyo katika njia ya kurejesha amani na uthabiti.

Tags