Sep 03, 2021 06:57 UTC
  • Algeria: Hatua za Morocco zimevuruga uhusiano wa pande mbili

Jeshi la Algeria limetangaza kuwa, hatua iliyochukuliwa hivi karibuni na serikali ya Algiers ya kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na Rabat ilikuwa uamuzi wa kiutawala na matokeo ya uchokozi wa Morocco.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Algeria imesema kuwa uchokozi huo wa Morocco umevuruga kabisa uhusiano wa pande mbili.

Gazeti la Rai Al-Youm linalochapishwa mjini London limeripoti kuwa, Kamandi ya Keshi la Algeria imeandika kuwa, uamuzi wa kukata uhusiano wa kidiplomasia na Morocco umechukuliwa baada ya muda mrefu wa uvumilivu na kustahamili vitendo vya kihasama na vya mara kwa mara vya serikali ya Morocco. 

Yapata wiki moja iliyopita Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Algeria alisema nchi hiyo imekata uhusiano wake wa kidiplomasia na Morocco.

Ramtane Lamamra amesema kuwa, Morocco imehusika na moto uliochoma misuti ya Algeria katika siku za karibuni na kwamba Algiers imeamua kukata uhusiano wake na Rabat.

Siku chache kabla yake Algeria iliuhusisha moto mbaya uliotokea hivi karibuni nchini humo na makundi mawili ambavyo imeyatambua kuwa ni magenge ya "kigaidi", na kusema kuwa moja ya kati ya makundi hayo liungwa mkono na kufadhiliwa na Morocco na Israeli.

Moto mkubwa wa misituni ulitanda eneo la Kaskazini mwa Afrika mwezi uliopita wa Agosti lakini umekuwa mkali zaidi nchini Algeria, ambako umesababisha uharibifu mkubwa na vifo vya makumi ya watu katika majimbo kadhaa haswa huko Tizi Ouzou katika mkoa wa Kabylie, mashariki mwa mji mkuu, Algiers.

Tags