Sep 04, 2021 06:47 UTC
  • Kipindupindu chaua zaidi ya watu 100 katika maeneo ya mpaka wa pamoja wa Niger na Nigeria

Wizara ya Afya ya Niger imetangaza kuwa, watu zaidi ya 100 wameaga dunia kwa ugonjwa wa kipindupindu ulioyakumba maeneo ya karibu na mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Nigeria.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini humo umesababisha vifo vya watu 104 kati ya watu 2,874 waliokumbwa na ugonjwa huo katika maeneo sita yaliyoko karibu na mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Nigeria.

Mnamo tarehe 19 ya mwezi uliopita wa Agosti, Wizara ya Afya ya Niger ilitangaza pia kuwa, watu 845 wamekumbwa na ugonjwa wa kipindupindu na 35 miongoni mwao wamefariki dunia katika mji mkuu wa nchi hiyo Niamey na maeneo mengine manne yaliyoko karibu na mpaka wa pamoja na Nigeria.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, mripuko wa kipindupindu umetokea pia katika eneo la Tillabéri kaskazini magharibi mwa nchi.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), wimbi la mwaka 2018 la mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Niger liliwakumba watu 3,824, ambapo 78 miongoni mwao walifariki dunia. Maeneo ya karibu na mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Nigeria ndiyo yaliyokuwa na maambukizi makubwa ya ugonjwa huo.../

Tags