Sep 04, 2021 07:41 UTC
  • Spika wa Bunge la Algeria: Kulikuwa na ulazima wa kuvunja uhusiano na Morocco

Spika wa Bunge la Algeria amesema, lilikuwa jambo lenye ulazima kwa nchi hiyo kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Morocco.

Salah Goudjil ameyasema hayo katika hafla ya kuanza kikao cha bunge la nchi hiyo kwa mwaka 2021-2022 na akabainisha kwamba, uamuzi wa Algiers kuvunja uhusiano wake na Rabat ulikuwa na ulazima.

Goudjil amesema, huko nyuma na kwa kzuingatia mambo mbalimbali, Algeria ilikuwa ikijitahidi kufumbia macho baadhi ya hatua za Morocco, lakini mara hii na baada ya Morocco kuandaa mazingira ya safari ya waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni wa Israel Yair Lapid mjini Rabat, ilimruhusu adui wa Algeria na nchi za Kiarabu kutoa kauli za vitisho dhidi ya Algiers akiwa katika ardhi ya nchi hiyo.

Kufuatia kushadidi mvutano baina ya nchi hizo mbili jirani za Kiarabu za Afrika Kaskazini huku ikiaminika kuwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umekuwa na nafasi katika kadhia hiyo, Algeria imechukua hatua ya kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Morocco ikiituhumu Rabat kuwa imehusika na hatua kadhaa za kiuadui na kiuhasama dhidi yake.

Kiwango cha sasa cha mivutano na mikwaruzano baina ya Algeria na Morocco hakijawahi kushuhudiwa kwa zaidi ya miaka 20.

Itakumbukwa kuwa nchi hizo mbili zenye mpaka wa pamoja wa nchi kavu wenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,700 na mambo mengi yanayoziunganisha pamoja kiutamaduni, ziliwahi pia kuvunja uhusiano wao kwa muda wa miaka 12 kuanzia mwaka 1976 hadi 1988.../  

Tags