Sep 05, 2021 11:52 UTC
  • Radiamali hasi ya vyama vya wafanyakazi Tunisia, kupinga uingiliaji wa Marekani

Vyama vya ushirika, vya wafanyakazi na vya kisiasa vya Tunisia, siku ya Jumatano vilisusia mazungumzo na ujumbe wa Marekani uliokwenda nchini humo kwa madai ya kutatua mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.

Vyama hivyo vilisusia kikamilifu kuonana na kuzungumza na timu ya maseneta wa Marekani waliojifanya kuwa wapatanishi wa mgogoro wa kisiasa wa Tunisia.

Chama chenye nguvu cha wafanyakazi kiitwacho UGTT na vyama viwili vya kisiasa vya Tunisia vilisema kuwa, vinapinga uingiliaji wowote wa kigeni katika kutatua migogoro ya ndani.

Chris Murphy, seneta wa chama tawala cha Democratic cha Marekani ndiye aliyongoza timu hiyo ya maseneta wa Marekani huko Tunisia na kufanya mazungumzo na Rais Kais Saied kuhusu mgogoro wa nchi hiyo. 

Msemaji wa Chama cha Wafanyakazi cha UGTT, Sami Tahri  amesema kuwa, masuala ya Tunisia yanapaswa kutatuliwa na Watunisia wenyewe bila ya uingiliaji wa kigeni.

Ususiaji na radiamali hasi ya vyama vikuu vya siasa na wafanyakazi nchini Tunisia dhidi ya uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo unaweza kutathminiwa katika pande kadhaa.

Rais Kais Saied wa Tunisia

 

Mosi ni kwamba uingiliaji huo wa Marekani unafanyika kwa sura ile ile ya kujifanya polisi wa dunia, kutojali haki ya kujitawala mataifa mengine na kulifanyia ubabe kila taifa. Dhati hiyo ya Marekani ilijitokeza kwa uwazi zaidi wakati wa urais wa Donald Trump.

Swali la wazi kabisa ni kwamba, kwa uthubutu gani Marekani imetuma timu yake ya maseneta huko Tunisia? Je, ni baada ya kupewa idhini na Umoja wa Mataifa au na Baraza la Usalama la umoja huo? Jawabu ni hapana. Je, Marekani imeombwa kufanya hivyo na serikali au vyama na taasisi husika za Tunisia? Jawabu ni hapana. Sasa imejipeleka huko kwa idhini ya nani? Kwa maneno mengine ni kwamba, kwa msingi na sheria ipi Marekani imejipa uthubutu wa kuingilia mgogoro wa kisiasa wa Tunsia bila ya kuombwa wala kupewa idhini na yeyote? Majibu yatakuwa ni yale yale kwamba Marekani inajifanya ni polisi wa dunia, haijali haki ya kujitawala mataifa mengine na inajiona iko juu ya mataifa yote duniani na inaweza kufanya inalotaka popote pale na wakati wowote ule.

Suala jengine ni kuwa, baada ya kukimbia kwa fedheha huko Afghanistan na kulifungulia njia kundi la Taliban kuidhibiti haraka na kiurahisi nchi hiyo, sasa hivi waitifaki wa Marekani wamepoteza mno imani yao kwa dola hilo la kibeberu na wanaamini kuwa wanaweza kupigwa teke na kusalitiwa wakati wowote na Marekani. 

Vile vile waitifaki wa Washington barani Ulaya walikuwa na tamaa kwamba kwa kuingia madarakani Joe Biden huko Marekani, wataweza kuimarisha zaidi ushirikiano wao na White House hasa kupitia shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO; ushirikiano ambao ulivurugwa vibaya na rais aliyepita wa Marekani, Donald Trump. Hata hivyo hivi sasa nchi hizo za Ulaya zinaona kwa mara nyingine Washington imeshindwa kuheshimu ahadi zake huko Afghanistan.

Seneta Chris Murphy wa Marekani

 

Sasa hivi timu ya maseneta wa Marekani imejipeleka nchini Tunisia kwa madai ya kutaka kutatua mgogoro wa nchi hiyo. Lakini uzoefu uliopatikana kutokana na uingiliaji wa kisiasa wa huko nyuma wa Marekani ikiwemo Afghanistan unaonesha wazi kuwa, Washington haina mwamana hata kidogo, haina uwezo wa kutatua mgogoro wowote ule, haiwezi kusimami jambo lolote inavyotakiwa na kuwasaliti ghafla waitifaki wake ni jambo jepesi sana kwake. Tajiriba hiyo inaonesha pia kuwa, hakuna chochote chenye thamani mbele ya Marekani isipokuwa maslahi yake binafsi tu. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana Watunisia wameamua kuususia ujumbe wa maseneta wa Marekani uliojipeleka nchini mwao bila ya hata kualikwa.

Inavyoonekana ni kuwa, wananchi wa Tunisia, vyama na taasisi zenye nguvu za nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika hawapendi na hawako tayari kukubali uingiliaji wa aina yoyote wa Marekani katika masuala yao ya ndani na waamini kuwa, hali ngumu iliyo nayo nchi yao hivi sasa inaweza kutatuliwa na Watunisia wenyewe bila ya uingiliaji wa madola ya kigeni.

Tunisia imeingia kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa baada ya rais wa nchi hiyo kumfuta kazi Waziri Mkuu na kulivunja Bunge.

Tags