Sep 07, 2021 01:22 UTC
  • Watu wasiopungua 30 wauawa katika shambulio kaskazini mashariki mwa Kongo

Duru za habari za kieneo na Umoja wa Mataifa jana Jumatatu ziliarifu kuwa, watu wasiopungua 30 waliuliwa katika shambulio la siku ya Jumaosi kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Duru hizo zimeongeza kuwa, waasi wa kundi la Allied Democratic Forces( ADF) wanashukiwa kutekeleza shambulio hilo katika eneo la Ituri. Kundi la ADF linaundwa na mamia ya magaidi wenye makao yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; eneo tajiri kwa madini mbalimbali. Hadi sasa waasi hao wametekeleza makumi ya mashambulizi makubwa dhidi ya raia wa mashariki mwa Kongo  tangu jeshi la nchi hiyo lianzishe oparesheni ya kuwasaka magaidi hao mwishoni mwa mwaka 2019.  

Magaidi wa ADF 

Maeneo ya mpakani ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  na Uganda, Rwanda na Burundi yanakabiliwa na makundi mbalimbali ya wanamgambo wenye silaha; na aghalabu ya wanamgambo hao ni wale waliobakia baada ya vita vikubwa vya ndani vilivyomalizika rasmi mwaka 2003.  

Umoja wa Mataifa unalituhumu kundi la waasi wa ADF kuwa limeuwa mamia ya raia tangu mwaka 2014. Mwaka 2017 kundi hilo lilitangaza utiifu wake kwa kundi la kigaidi la Daesh. 

Tags