Sep 08, 2021 11:50 UTC
  • Sudan yamwita kumsaili balozi wa Ethiopia baada ya miili 29 kupatikana katika Mto Setit

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan imemwita kwa ajili ya kumsaili balozi wa Ethiopia mjini Khartoum baada ya miili 29 inayosadikiwa kuwa ni ya Watigray kupatikana katika Mto wa Setit.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan imeeleza kuwa, viwiliwili hivyo 29 vilivyookotwa katika mto Setit ambao nchini Ethiopia unajulikana kama Mto Tekeze vimetambuliwa kuwa ni vya Waethiopia kutoka jimbo la Tigray.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan imeeleza kuwa, viwiliwili hivyo viliokotwa kando kando ya mto huo kati ya Julai 26 na Agosti 8 mwezi uliopita.

Dina Mufti, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ethiopia bado hajatoa radiamali yoyote kuhusiana na taarifa hii.

Mivutano baina ya nchi mbili jirani za Ethiopia na Sudan zimechukua wigo mpana zaidi katika miezi ya hivi karibuni zikivutana kuhusiana na masuala mbalimbali kubwa zaidi likiwa mzozo wa mpaka na mgogoro wa ujenzi w Bwawa la al-Nahdha.

Dina Mufti, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ethiopia

 

Mwezi uliopita mzozo huo uliingia katika hatua mpya baada ya Serikali ya Sudan kumwita nyumbani balozi wake mjini Addis Ababa ikipinga madai yaliyotolewa na Ethiopia kwamba Khartoum inaingilia mgogoro wa eneo la Tigray.

Wasiwasi katika mpaka wa Sudan na Ethiopia uliongezeka baada ya kutokea mapigano katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka jana (2020). Zaidi ya wakimbizi 50 elfu wa Ethiopia walikimbilia katika maeneo ya mashariki mwa Sudan kukwepa mapigano hayo.

Tags