Sep 09, 2021 11:09 UTC
  • Ramtane Lamamra
    Ramtane Lamamra

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Algeria imetilia mkazo msimamo wake wa kuendelea kutetea taifa la Palestina na kupinga uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya Syria na Libya.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Algeria imesema kuwa, katika safari yake ya Cairo huko Misri ambako anashiriki mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Ramtane Lamamra, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria atajadiliana na wenzake kuhusu hali ya kisiasa ya Syria, Libya, Palestina, Yemen, mapambano dhidi ya ugaidi na suala la kuangamiza silaha za mauaji ya halaiki na kwamba lengo la kushiriki Algiers katika mkutano huo ni kusisitiza msimamo wa nchi hiyo wa kulitetea taifa la Palestina, kutumia mazungumzo kama njia ya kutatua migogoro katika nchi mbalimbali za Kiarabu na kupinga aina zote za uingiliaji kati wa madola ya kigeni. 

Baraza la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu linakutana leo mjini Cairo chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Kuwait Ahmed Nasser Al-Mohammed Al-Sabah.Arab Leaguue

Mkutano wa Jumuiya ya Kiarabu

Algeria imekuwa mstari wa mbele kati ya nchi za Afrika katika kutetea haki za watu wanaodhulumiwa wa Palestina. Siku chache zilizopita pia Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Algeria, Ramtane Lamamra alisema nchi hiyo itaendeleza jitihada katika Umoja wa Afrika za kufutwa hadhi ya mwanachama mwangalizi iliyopewa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), Moussa Faki Mahamat wa kuipatia Israel hadhi ya mwanachama mwangalizi katika AU umezusha utata mkubwa baina ya nchi za Afrika.

Nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Afrika zimetangaza rasmi kuwa zinataka uamuzi wa kuipa Israel hadhi ya mwangalizi katika umoja huo ubatilishwe ili kulinda heshima na nafasi ya Umoja wa Afrika.

Tags