Sep 13, 2021 11:09 UTC
  • Viongozi wa Kiislamu Kenya: Visa vya kupotezwa washukiwa vimeongezeka

Viongozi wa Kiislamu nchini Kenya wameishutumu serikali kwa kuongezeka kwa visa vya kupotezwa washukiwa wa ugaidi nchini humo.

Baraza Kuu la Waislamu nchini Kenya (Supkem), Muungano wa Jamii ya Wasomali, mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na Seneta Mohammed Faki wameitaka serikali ya Kenya iwe ikiwapeleka kortini washukiwa.

Wakizungumza mjini Mombasa, wamesema kutoweka kwa mfanyabiashara Abdulhakim Salim Sagar kumeibua maswali mengi. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Bw Manase Mwania Musyoka amesema Bw Sagar, ambaye anahusishwa na ugaidi, hakukamatwa na kitengo chochote cha Huduma ya Polisi ya Kitaifa (NPS).

Bw Musyoka alikana kufahamu lolote kuhusu kukamatwa kwa mshukiwa huyo na maafisa wa polisi.

Hata hivyo familia ya Sagar inalishutumu Jeshi la Polisi la Kenya kwa kushindwa kutoa maelezo ya mahali alipo mshukiwa huyo.

Mwezi uliopita baadhi ya vyombo vya habari vya Kenya viliripoti kuwa, mfanyabiashara huyo wa Mombasa anayekabiliwa na mashtaka ya ugaidi kutekwa nyara na watu wasiojulikana wanaoshukiwa kuwa maafisa kutoka Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi (ATPU).

Bw Sagar, 40, alitekwa nyara na watu wasiojulikana akirudi nyumbani kutoka msikitini mwendo wa saa kumi na mbili jioni huko eneo la Kule mjini Old Town.

Familia yake inadai kuwa, Bw Sagar alikuwa amepokea vitisho kabla ya kutekwa kwake nyara. Sagar alikuwa na kesi ya ugaidi katika Korti ya Shanzu na amekuwa akiripoti kwa mpelelezi mara moja kwa mwezi.

Baadhi ya walioteweka kwa kutekwa nyara nchini kenya ni Abdulhakim Salim Sagar (Mombasa), Prof Abdiwahab Sheikh (Nairobi), Yassir Ahmed (Lamu), Alfani Juma (Mombasa) na Abdisatar Islam (Mombasa).

Tags