Sep 14, 2021 12:26 UTC
  • Rais Samia Suluhu Hassan
    Rais Samia Suluhu Hassan

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezitaka mamlaka zinazoshughulikia zoezi la sensa lililopangwa kufanyika mwakani kutumia gharama ndogo na kufanya zoezi hilo kwa ufanisi kwani serikali haina pesa ya kubeba gharama kubwa.

Rais Samia amesema hayo leo Jumanne, Septemba 14, 2021 wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya uelimishaji na uhamasishaji kuhusu sensa ya mwaka 2022 iliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametilia mkazo kuwa, suala la Sensa linatambulika kwenye dini zetu zote mbili na viongozi wetu wa dini wameyasema hayo na kwamba suala hilo linadhihirisha kuwa Sensa imekuwepo duniani kwa miaka mingi. Amesema, Sensa ya kwanza nchini Tanzania ilifanyika mwaka 1910 wakati wa utawala wa Ujerumani, ili kufahamu nguvu kazi iliyopo nchini humo. Ameongeza kkuwa Sensa ya kwanza ya kisayansi ilifanyika mwaka 1967 baada ya Tanganyika na Zanzibar kupata uhuru na kuungana.

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wasimamizi wa Sensa hiyo wajitahidi kutumia mbinu na nyenzo zote kuwafikia wananchi kote waliko na kwa rika zote, ikiwemo vipindi vya radio na televisheni, magazeti, wasanii na wanamuziki, njia za TEHAMA kupitia mitandao ya kijamii, meseji za simu, n.k.

Amesema taarifa za Sensa zitasaidia kufahamu ongezeko la idadi ya watu, hali ya uhamiaji, mfano kutoka vijijini kwenda mijini na wale wanaotoka nje ya nchi, pia kupima maendeleo yaliyofanyika tangu Sensa ya mwisho.

Tags