Sep 15, 2021 12:43 UTC
  • Vyama vitano vya siasa Tunisia vyapinga amri ya rais ya kusitishwa Katiba

Vyama 5 vya siasa nchini Tunisia vimetoa taarifa ya pamoja vikipinga amri ya kusitishwa Katiba na kufanyiwa mageuzi.

Katika taarifa hiyo vyama hivyo vitano vya Tunisia vimetangaza kuwa, vinapinga suala la kusitishwa Katiba au kufanyiwa marekebisho na vimemtaka Rais Kais Saeid wa nchi hiyo aheshimu majukumu yake mbele ya taifa, kutekeleza Katiba na kuheshimu kiapo alichokula kabla ya kushirika wadhifa huo.

Taarifa hiyo pia imelaani ukiukwaji wa mara kwa mara wa haki na uhuru wa kimsingi wa raia ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza na kuhukumiwa raia katika mahakama za kijeshi na imemtaja Rais Kais Saeid kuwa ndiye anayepaswa kuwajibika kuhusiana na uhalifu huo. 

Maandamano ya wananchi dhidi ya serikali Tunisia

Taarifa hiyo ya vyama vitano vya upinzani nchini Tunisia imetolewa baada ya Mshauri wa Rais wa Tunisia, Walid El Hajjam kusema kuwa, Katiba ya sasa ya nchi hiyo ni kikwazo kikubwa na kwamba inapaswa kusitisha na kuanzishwa mfumo wa muda wa utawala nchini humo. El Hajjam alisisitiza kuwa Rais wa Tunisia ataanza kutekeleza mipango yake mipya hivi karibuni. 

Januari 25 mwaka huu Rais wa Tunisia alimfuta kazi Waziri Mkuu, Hicham Mechichi na kusitisha shughuli za bunge sambamba na kuwaondolea wabunge kinga ya kisheria baada ya kupamba moto mgogoro wa kisiasa nchini humo.   

Tags