Sep 17, 2021 02:41 UTC
  • Mgogoro wa ndani Somalia wanazidi kutokota baada ya Rais kubana madaraka ya Waziri Mkuu

Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Mohamed amesimamisha madara ya Waziri Mkuu, Mohammed Hussein Roble ya kuajiri na kuwafuta kazi maafisa wa serikali, suala ambalo linachochea kuni katika ugomvi na mivutano inayoendelea kushuhudiwa sasa baina ya makundi ya kisiasa ya Somalia.

Mzozo kati ya viongozi hao wawili unaashiria kuongezeka kwa mivutano ya miezi kadhaa ambayo inatishia kukwamisha mchakato wa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais wa Somalia imesema: "Waziri Mkuu amekiuka katiba ya mpito kwa hivyo mamlaka yake ya utendaji yanaondolewa, haswa mamlaka ya kufuta na kuteua maafisa, hadi uchaguzi utakapokamilika."

Hadi tunatayarisha habari hii hakuna taarifa yoyote iliyokuwa imetolewa na Waziri Mkuu wa Somalia, Mohammed Hussein Roble kuhusiana na hatua hiyo ya Rais Mohamed Abdullahi Mohamed Farmaajo.

Mohammed Hussein Roble

Kipindi cha utawala wa miaka minne wa Farmaajo kilimalizika mwezi Februari mwaka huu, lakini kilirefushwa na Bunge mwezi wa Aprili, na kusababisha mapigano makali ya silaha katika mji mkuu waSomalia, Mogadishu.  Wapinzani wa kiongozi huyo waliitaja hatua hiyo kuwa ni unyakuzi wa madaraka.

Uchaguzi nchini Somalia unafuata mtindo tata ambapo mabunge ya majimbo na wajumbe wa koo za nchi hiyo huchagua wabunge wa Bunge la Taifa, ambao kwa upande wao humchagua Rais wa nchi.

Mchakato huo umepangwa kufanyika baina ya Oktoba Mosi hadi tarehe 25 Novemba mwaka huu.