Sep 17, 2021 11:24 UTC
  • William Ruto: Niko tayari kuzungumza na Rais Kenyatta bila masharti

William Ruto, Naibu Rais wa Kenya amesema kuwa, yuko tayari kumaliza msuguano uliojitokeza kati yake na Rais Uhuru Kenyatta bila ya masharti yoyote.

Mvutano kati ya Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto, siyo suala la siri ni taswira ambayo imekuwa ikionekana wazi. Katika hali ambayo, Rais Uhuru Kenyatta anadai kwamba  hafahamu chanzo chake, William Ruto amekuwa akimnyoshea kidole cha lawama kinara wa chama cha ODM Raila Odinga akisema kwamba, Waziri Mkuu huyo wa zamani ndio chanzo cha kuvurugika uhusiano wake na Rais Kenyatta.

Uhasama kati ya viongozi hao wa ngazi za juu nchini Kenya umesababisha hali ya hofu katika taifa ambalo linakaribia kufanya uchaguzi na lenye historia ya machafuko kila wakati uchaguzi unapoandaliwa. Ruto anakua wa kwanza kuitikia  wito wa maaskofu wa kanisa katoliki unaotaka kufikia maridhiano.

Raid Odinga kiongozi wa ODM anayelalamikiwa kuwa chanzo cha kuharibika uhusiano wa Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto

 

Mwezi uliopita Rais Uhuru Kenyatta alimtaka Naibu wake ajiuzulu kama haridhishwi na utendaji kazi wa serikali. Kiyume chake  Ruto aliapa kwamba hatojiuzulu kwani hatua hiyo ingemwonesha kuwa mwanasiasa  mwoga na msaliti. 

Uhasama kati ya Rais Kenyatta na Naiabu wake William Ruto  ulichukua mkondo mpya wakati Rais wa Kenya, aliposalimiana na hasimu wake wa kisiasa Raila Odinga mwezi Machi mwaka 2018 kwenye tukio maarafu lililofahamika kama hendisheki baada ya kuzika tofauti zao baada ya uchaguzi mkuu uliokuwa na utata uliofanywa mwaka 2017, ambapo Raila alidai kuwa aliibiwa kura.