Sep 17, 2021 11:26 UTC
  • Tanzania yatahadharisha kuhusu mlipuko wa Homa ya uti wa mgongo

Serikali ya Tanzania imewataka wananchi wan chi hiyo ya Afrika Mashariki kuchukua tahadhari kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo uliotokea katika jimbo la Tshopo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale, imesema kuwa, ni vyema kuendelea kuchukua tahadhari kwani magonjwa hayana mipaka, hususani mikoa ya Tanzania inayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ikiwemo Kigoma, Rukwa, Kagera, Katavi na Songwe.

“Ugonjwa huu huchukua siku mbili hadi 10 tangu kuambukizwa hadi kuanza kuonyesha dalili,” amesema Dk  Sichwale.

Aidha Mganga Mkuu wa serikali ya Tanzania amesema kuwa, wizara inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa ugonjwa huo nchini DRC na kuchukua hatua ili kuzuia na kujiandaa kukabiliana na tishio la ugonjwa huo endapo utajitokeza nchini Tanzania.

Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Tanzania

 

Vimelea vya ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya hewa au kukaa na mtu mwenye maambukizi, kulingana na wataalamu wa magonjwa sugu ya kuambukizwa.

Mlipuko wa Homa ya uti wa mgongo ni tishio kwa sasa barani Afrika, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa Septemba 8, 2021 na Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika.

Wataalamu wanasema kuwa, dalili kuu za ugonjwa huu ni pamoja na homa kali, kichwa kuuma, kutapika, kuogopa mwanga, kuchanganyikiwa na shingo kukakamaa.