Sep 19, 2021 16:34 UTC
  • Wafanyamapinduzi Guinea wakataa wito wa kuachia madaraka, wasema hawababaishwi na vikwazo

Kundi la wanajeshi waliotwaa madaraka ya nchi huko Guinea kupitia mapinduzi limepinga mashinikizo ya kimataifa yanayotaka kuachiliwa huru rais wa zamani wa nchi hiyo aliyeshikiliwa kizuizini, Alpha Conde na kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.

Kanali Mamady Doumbouya, ambaye alitwaa madaraka nchini Guinea mnamo Septemba 5, ameuambia ujumbe wa viongozi wa Afrika Magharibi kwamba hababaishwi na vikwazo vipya vilivyowekwa na jumuiya ya kikanda ya ECOWAS ili kushinikiza mabadiliko ya haraka ya utawala wa kikatiba.

Kanali Mamady Doumbouya ameyasema hayo baada ya wawakilishi wawili kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) kukutana na kiongozi huyo mpya mjini Conakry siku ya Ijumaa iliyopita. Jumuiya hiyo yenye wanachama 15 imeamua kuzuia fedha za kundi la wanajeshi waliofanya mapinduzi dhidi ya serikali na za jamaa zao na kuwazuia kusafiri nje ya nchi.

Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara na mwenzake wa Ghana Nana Akufo-Addo, ambao walifanya ziara ya siku moja katika mji mkuu wa Guinea, walimtaka kiongozi huyo wa mapinduzi kumwachilia huru Conde na kuitisha uchaguzi mpya katika kipindi cha miezi sita.

Alpha Conde anashikiliwa na wanajeshi waliofanya mapinduzi Guinea

Hata hivyo kanali Doumbouya amekataa wito huo na kuwaambia wawakilishi wa ECOWAS kuwa, kuachiliwa huru Conde ni kinyume na matakwa ya wananchi.

Doumbouya amewaambia wajumbe hao kwamba "ni muhimu kwa ECOWAS kusikiliza matakwa halali ya watu wa Guinea."

Mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea yameendelea kulaaniwa kieneo na kimataifa huku kukitolewa miito ya kuachiliwa huru Rais Alpha Conde anayeshikiliwa kizuizini na wanajeshi waliofanya mapinduzi.

Tags