Sep 20, 2021 02:24 UTC
  • Choguel Kokalla Maïga
    Choguel Kokalla Maïga

Waziri Mkuu wa Mali amesema kuwa, nchi hiyo ina haki ya kuomba msaada na himaya ya kijeshi kutoka kwa mtu yeyote imtakaye.

Choguel Kokalla Maïga, Waziri Mkuu wa Mali amesema hayo akijibu matamshi ya Ufaransa ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi na maamuzi ya serikali ya Bamako na kusisitiza kwamba, nchi hiyo ina uhuru kamili wa kujichukulia maamuzi na kuomba msaada hata wa kijeshi kutoka popote.

Serikali ya Mali imekasirishwa na madai ya serikali ya Ufaransa kwamba, hatua ya serikali ya Bamako ya kuomba msaada wa kijeshi kutoka kwa mataifa mengine ilihali vikosi vya Ufaransa vipo katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika si kitendo kinachofaa.

Hata hivyo Waziri Mkuu wa Mali amesisitiza kwamba, serikali ikitaka kuomba msaada wa kijeshi kutoka kwa nchi yoyote inaweza kufanya hivyo na kwamba, Ufaransa haina haki ya kuingilia maamuzi ya serikali ya nchi hiyo ya kiafrika. 

Wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali

Wananchi wa Mali wamekuwa wakifanya maandamano mara kwa mara wakipinga uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo.

Wanajeshi wa Ufaransa walielekea Mali katikati ya mwaka 2013 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, hata hivyo magaidi wangali wanafanya hujuma za mara kwa mara nchini humo licha ya uwepo wa wanajeshi hao wa Ufaransa, huku magaidi wakishadidisha mashambulizi na jinai kutokea Mali hadi katika nchi za Niger na Burkina Faso.