Sep 21, 2021 07:57 UTC
  • Jaribio la kuipindua serikali ya Sudan lazimwa

Serikali ya Sudan imetangaza kuwa imetibua na kuzima jaribio la mapinduzi la kuiangusha serikali hiyo na kutoa mwito kwa wananchi kuwa watulivu sambamba na kuwahakikishia kuwa inadhibiti hali ya mambo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, waliohusika katika jaribio hilo la mapinduzi walitaka kudhibiti kituo cha radio ya taifa hata hivyo hawakufaulu.

Vyombo vya habari vya serikali vimesema: "kulikuwa na jaribio la mapinduzi lililoshindwa, lazima watu wakabiliane nalo,". 

Kwa mujibu wa duru hizo za habari waliopanga njama walijaribu kudhibiti jengo la shirika la utangazaji la serikali, lakini "hawakufaulu."

Msemaji wa serikali amesema zoezi la kuwahoji wanaoshukiwa kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi litaanza muda mfupi ujao.

Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok

Wiki iliyopita zilisambaa tetesi za kufanyika jaribio la mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan. Hata hivyo jeshi lilikadhibisha taarifa hizo zilizotangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba wanajeshi wa nchi hiyo walikuwa wakila njama ya kufanya mapinduzi nchini humo; na kwa mara nyingine tena likatangaza kuwa linaheshimu na kufungamana na wajibu wake wa kuilinda nchi na serikali ya mpito ya nchi hiyo.

Kwa sasa Sudan inaendeshwa kwa mkataba na makubaliano ya kugawana madaraka kati ya wanajeshi na raia kufuatia kupinduliwa rais wa zamani Omar al-Bashir mnamo Aprili 2019.../

Tags