Sep 21, 2021 08:56 UTC
  • Kuendelea mgogoro wa Tunisia; maandamano ya waungaji mkono na wapinzani wa maamuzi ya Rais

Mgogoro wa Tunisia umechukua wigo mpana zaidi hivi sasa ambapo waungaji mkono na wapinzani wa maamuzi ya Rais Kais Saied wa nchi hiyo wamemiminika katika mitaa na barabaraza za miji ya nchi hiyo.

Akthari ya waandamanaji hao walisikika wakipiga nara dhidi ya maamuzi ya Rais na kutoa wito wa kuanza tena shughuli za Bunge. Katika upande wa pili, kundi jingine la waandamanaji hao lilipiga nara za kuunga mkono hatua na maamuzi yaliyochukuliwa na Rais wa Tunisia, na hivyo kufanya mudhahara na maandamano hayo kutawaliwa na kambi mbili za wapinzani na waungaji mkono.

Katika maandamano ya juzi, wapinzani walitangaza kuwa, maamuzi yaliyochukuliwa na Rais Kais Saied Julai 25 mwaka huu yalikuwa ni mapinduzi dhidi ya katiba ya nchi na hivyo wametoa wito wa kushtakiwa katika mahakama ya kijeshi. Aidha wamelaani kile walichokitaja kuwa kurejea udikteta katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Kile kilicho dhahir shahir ni kuwa, mgogoro wa kisiasa nchini Tunisia umechukua wigo mpana zaidi. Mgogoro huo uliibuka kufuatia hatua ya wananchi ya kulalamikia mazingira mabaya ya kiuchumi na kisiasa yanayotawala katika nchi hiyo. Malalamiko hayo, yalimfanya Rais Kais Saied amemfute kazi Waziri Mkuu, Hichem Mechichi na kusitisha shughuli za bunge sambamba na kuwaondolea wabunge kinga ya kisheria baada ya kupamba moto mgogoro wa kisiasa nchini humo.   

Hatua hiyo kama ilivyotarajiwa ilikabiliwa na upinzani mkali mwanzoni tu mwa kutangazwa kwake ambapo vyama, makundi na mirengo mbalimbali ya kisiasa ikiwemo Harakati ya Nahadha ilijitokeza na kulalamikia uamuzi huo. Wapinzani wa Rais Kais Saied walitangaza kuwa, maamuzi hayo yanakinzana bayana na mwenendo wa kidemokrasia nchini humo na ndio maana wakamtaka Rais atazame upya uamuzi huo na aruhusu shughuli za Bunge ziendelee kama kawaida. Katika kutetea maamuzi yake, Rais Kais Saied alisema kuwa, kuna kundi la watenda jinai ambalo limewafanya wananchi wa Tunisia wabakie na njaa na kuhodhi uchumi wa nchi kwa ajili ya maslahi yao hatua ambayo imeufanya ufisadi kuenea katika kona zote za nchi hiyo.

Rais Kais Saied wa Tunisia

 

Rais Kais ambaye kwa sasa anashirikia hatamu za uongozi wa mihimili yote mikuu ya dola amesisitiza kuwa, katu hatalegeza kamba katika njia hiyo na ana azma thabiti ya kuleta mageuzi ya kimsingi katika mfumo wa kisiasa wa nchi. Kutokana na msimamo huo, pande za ndani na za kieneo zinamtaka Rais wa Tunisia aharakishe mwenendo wa kuunda serikali na kuweka wazi mipango yake ili kuiondoa haraka nchi hiyo katika mgogoro wa Katiba. Ukweli wa mambo ni kuwa, kuendelea kwa hali hii kumewafanya akthari ya wananchi wa Tunisia wahisi hatari. Kwa mtazamo huo ni kuwa, kuendelea hali hii yumkini kukaufanya mfumo unaotawala hivi sasa nchini humo kukosa uhalali na kwa mara nyingine tena kurejea udikteta katika nchi hiyo.

Akthari ya wapinzani nchini Tunisia wametoa indhari kuhusiana na kamatakamata inayofanywa na vyombo vya dola dhidi ya wapinzani pamoja na muamala mbaya dhidi yao pamoja na kuongezeka uingiliaji wa kigeni katika nchi hiyo.

Eric Goldstein, Mkurugenzi wa Asia Magharibi na Kaskazini mwa Afrika wa Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch sambamba na kukosoa  siasa za ukandamizaji za Rais Kais Saied amesema kuwa, ukandamizaji wenye matashi ya kisiasa wa Rais wa Tunisia umeongezeka tangu Julai 25 mwaka huu wakati alipositisha shughuli za Bunge.

Rachid al-Ghannouchi, Kiongozi wa Harakati ya al-Nahdha

 

Rachid al-Ghannouchi, Kiongozi wa Harakati ya al-Nahdha sanjari na kuashiria kwamba, kuweko mazungumzo yasiyo na mpaka ni njia bora na mwafaka kwa ajili ya kupatia ufumbuzi mambo yote amesema kuwa, nina matumaini wachezaji wakuu na muhimu wa kisiasa nchini Tunisia watakutana kwa ajili ya kutayarisha uwanja wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa chini ya usimamizi wa Rais Kais Saied kwa minajili ya kutafuta njia za kuikwamua nchi hiyo katika kinamasi na mgogoro ambao imekwama ndani yake. Pamoja na hayo, matakwa ya vyama vya siasa nchini Tunisia yametupiliwa mbali.

Rais Kais Saied ametangaza habari ya kufanya mageuzi ya katiba katika fremu ya  kuboresha mazingira ya kisiasa, kung'oa mizizi ya ufisadi na kurahisisha mwenendo wa kidemokrasia katika nchi hiyo, anasisitiza kuwa, sisi siyo wafuasi wa vurugu na machafuko na kwamba, wananchi wana haki ya kubainisha maoni na mitazamo yao kwa uhuru kamili. Sisi hatuwaogopi watu ambao wameisaliti nchi yao na kuvunja makubaliano.

Pamoja na hayo, kupita muda mrefu na kutofahamika maamuzi ya Rais wa Tunisia, kubinywa uhuru wa kisiasa na kusimamishwa kwa muda mrefu shughuli za Bunge ni mambo ambayo yamezusha wasiwasi kuhusiana na mustakabali wa kisiasa wa Tunisia ndani na nje ya nchi hiyo. Kwa msingi huo basi, siku za usoni huko nchini Tunisia zitakuwa muhimu mno katika mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Tags