Sep 21, 2021 11:56 UTC
  • Kiongozi wa zamani wa kijeshi wa Misri afariki dunia akiwa na miaka 85

Kiognozi wa zamani wa kijeshi wa Misri amefariki dunia leo Jumanne akiwa na umri wa miaka 85. Field Marshal Mohammed Hussein Tantawi aliiongoza kwa muda na kipindi kifupi Misri mwaka 2011 baada ya wananchi kumpindua Rais Hosni Mubarak.

Tantawi alishiriki kwenye vita dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika miaka ya 1956, 1967 na 1973. Alikuwa waziri wa ulinzi wa Misri kwa muda wa miaka 21.

Tantawi alipokonywa uwaziri wa ulinzi mwezi Agosti 2012 wiki chache baada ya Rais Mohammed Morsi kuingia madarakani kwa njia ya kura za wananchi. Huyo alikuwa rais wa kwanza wa Misri kuwahi kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo lakini alipinduliwa na Jenerali Abdul Fattah el Sisi, rais wa hivi sasa wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Tantawi alikuwa mkuu wa baraza la kijeshi lililoongoza Misri kwa muda wa mwaka moja na nusu baada ya kumuondoa madarakani kwa nguvu Rais Hosni Mubarak mwezi Februari 2011.

Field Marshal Mohammed Hussein Tantawi 

 

Baada ya kushadidi maandamano ya wananchi wa Misri mwaka 2011, Tantawi aliongoza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Hosni Mubarak, lakini yeye mwenyewe naye alipokonywa cheo chake cha zaidi ya miongo miwili cha waziri wa ulinzi, mara baada ya Rais Muhammad Morsi kuingia madarakani.

Field Marshal Tantawi alizaliwa mwaka 1935, asili yake ni Mnubi na aliingia jeshini mwaka 1956. Mwaka 1991 Tantawi alishiriki kwenye vita vilivyoongozwa na Marekani dhidi ya Saddam Hussein kwa ajili ya ukombozi wa Kuwait.

Baada ya kupokonywa uwaziri wa ulinzi, Tantawi alipotea sana katika macho ya watu na alionekana mara moja moja kama katika sherehe za uzinduzi wa Mfereji mpya wa Suez mwaka 2015.