Sep 21, 2021 13:25 UTC
  • Waziri Mkuu wa Sudan: Wapangaji wa mapinduzi walikuwa ndani na nje ya jeshi

Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok amesema leo Jumanne kuwa jaribio lililoshindwa la mapinduzi liliandaliwa na watu ndani na nje ya jeshi la nchi hiyo.

Hamdok amesema kuwa "kwa mara ya kwanza, watu waliohusika katika jaribio hilo wamekamatwa," na kwamba hapo awali pia kulifanyika majaribio ya kuvuruga usalama, haswa mashariki mwa Sudan.

Mapema Jumanne ya leo, serikali ya Sudan ilisema kwamba maafisa wa jeshi na raia wenye uhusiano na utawala ulioondolewa madarakani wa Omar al-Bashir walifanya jaribio la mapinduzi lakini walidhibitiwa haraka.

Msemaji wa serikali ya Sudan, Mohamed al-Faki Suleiman amesema washukiwa wa jaribio la mapinduzi walikuwa wakiendelea kusailiwa baada tu ya baadhi yao kutiwa nguvuni. 

Sudan imekuwa katika pandashuka nyingi za kurejesha utawala wa kidemokrasia nchini humo tangu mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani mtawala wa muda mrefu wa nchi hiyo, Omar al-Bashir  Aprili 2019, kufuatia maandamano ya wananchi ya miezi minne.

Rais wa Sudan aliyeng'olewa madarakani, Omar al Bashir 

Wiki iliyopita zilisambaa tetesi za kufanyika jaribio la mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan. Hata hivyo jeshi lilikadhibisha taarifa hizo zilizotangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba wanajeshi wa nchi hiyo walikuwa wakila njama ya kufanya mapinduzi nchini humo; na kwa mara nyingine tena likatangaza kuwa linaheshimu na kufungamana na wajibu wake wa kuilinda nchi na serikali ya mpito ya nchi hiyo.

Tags