Sep 22, 2021 13:37 UTC
  • Mahakama ya Tanzania yamfutia mashtaka ya uchochezi Tundu Lissu na wenzake watatu

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es salaam, Tanzania imefuta mashtaka dhidi ya makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu na wenzake watatu, baada ya upande wa mashtaka wa serikali ya nchi hiyo kutangaza leo kuwa hauna nia tena ya kuendelea na mashtaka yote matano uliyokuwa umefungua dhidi ya washtakiwa hao.

Mwaka 2016, Tundu Lissu na wahariri wa gazeti la MAWIO Jabir Idrissa na Simon Mkina pamoja na Ismail Mehboob, aliyekuwa meneja wa kiwanda cha uchapishaji cha Flint, walifunguliwa mashtaka ya uchochezi katika kesi ya jinai namba 208/2016.

Katika kesi hiyo, makamu huyo mwenyekiti wa Chadema na wenzake hao walikuwa wanatuhumiwa kwa mashtaka matatu ya uchochezi, likiwemo la kutoa chapisho la uchochezi kwenye gazeti la Mawio, toleo Na. 182 la tarehe 14 hadi 20 Januari, 2016.

Shtaka jingine dhidi ya Lissu na wenzake lilikuwa ni kupanga njama za kutoa chapisho la uchochezi, kosa walilodaiwa kutenda kati ya tarehe 12 na 14 Januari 2016 katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam; na Lissu na wahariri wa Mawio wakadaiwa kupanga njama pia za kuchapisha taarifa za uchochezi.

Shtaka jengine lilikuwa ni kuchochea hofu miongoni mwa wananchi kwa kuchapisha habari "Maafa yaja Zanzibar" ambapo ilidaiwa kwamba habari hiyo ingeweza kuzua vita au umwagaji damu.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania

Ikumbukwe kuwa tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani nchini Tanzania mnamo mwezi Machi 2021 kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo John Pombe Magufuli, mahakama ya nchi hiyo imeshafuta kesi kadhaa ikiwemo kesi maarufu ya Mashekhe wa Uamsho wa Zanzibar, ambazo weledi wengi wa masuala ya kisheria na kisiasa nchini humo wamekuwa wakisisitiza kwamba zimechangiwa zaidi na sababu za kisiasa.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa imechangiwa zaidi na agizo la mara kwa mara la rais Samia kuvitaka vyombo vya dola likiwemo jeshi la Polisi na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa, TAKUKURU zifute kesi za muda mrefu zisizo na ushahidi zikiwemo za ubambikizaji, ambazo zimesababisha magereza ya nchi hiyo kurundika idadi inayokaribiana ya wafungwa na mahabusu wanaongojea kusikilizwa kesi zao.../

Tags