Sep 23, 2021 04:13 UTC
  • Bunge la Libya lapiga kura ya kutokuwa na imani na Baraza Kuu la Serikali ya nchi hiyo

Bunge la Libya limepiga kura ya kutokuwa na imani na Baraza Kuu la Serikali ya nchi hiyo. Hatua hiyo imecukuliwa huku pande zote zinazozozana nchini Libya zikiwa mbioni kutayarisha mazingira mwafaka ya kuitisha uchaguzi huru na wa haki nchini humo na kukomesha mgogoro unaoendelea kwa zaidi ya miaka 10 sasa katika nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Bunge la Libya, Abdallah Bilhaq imesema kuwa, wabunge 89 kati ya 113 wa bunge hilo lililoko Tobruk wamepitisha uamuzi wa kutokuwa na imani na serikali ya mpito. Hata hivyo msemaji wa serikali ya mpito ya Libya amesema uamuzi huo wa Bunge la Tobruk ni batili na unapingana na Katiba ya Libya. 

Uamuzi huo umechukuliwa baada ya makundi na vyama vya siasa nchini Libya kufikia mwafaka kwa ajili ya kuitisha chaguzi za Rais na Bunge ambazo zimepangwa kufanyika tarehe 24 mwezi Disemba. Juhudi za kutafuta suluhisho la mgogoro wa ndani wa Libya zimekuwa zikiendelea kwa miezi kadhaa sasa katika mazungumzo yanayoshirikisha makundi ya kisiasa na kupitia vikao na mikutano inayofanyika kwa upatanishi wa nchi mbalimbali na chini ya mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa. Mazungumzo na vikao hivyo vimesaidia kutayarisha uwanja mzuri wa kuwepo maelewano ya kiwango fulani baina ya makundi mbalimbali ya Libya yaliyopelekea kubuniwa sheria za uchaguzi ujao. 

Katika mkondo huo, siku chache zilizopita Spika wa Bunge la Libya, Aguila Saleh alisaini nakala ya mwisho ya sheria ya uchaguzi nchini humo. Hata hivyo hatua hiyo imeandamana na upinzani mkubwa hususan wa Baraza Kuu la Utawala wa Libya. Sheria hiyo inawaruhusu maafisa wa sasa wa serikali ya mpito kugombea katika uchaguzi ujao kwa sharti kwamba wawe wamejiuzulu nyadhifa zao miezi mitatu kabla ya uchaguzi.

Aguila Saleh

Baraza Kuu la Serikali ya Libya (serikali ya mpito) limepinga hatua ya Aguila Saleh ya kusaini sheria hiyo na kutangaza kuwa, Spika huyo wa Bunge ana nia ya kukwamisha zoezi la uchaguzi kutokana na kusaini kwa makusudi sheria nakisi na yenye mapungufu ya uchaguzi. 

Alaa kulli hal, mzozo huo umezidisha mivutano baina ya makundi ya kisiasa nchini Libya. Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwepo mjadala wa kusailiwa serikali ya mpito ya nchi hiyo kwa hoja kwamba, haijachukua hatua za kutosha. Wawakilishi wa Bunge la Libya wanaamini kuwa, serikali ya mpito haijachukua hatu za kutosha katika jitihada za kufanikisha maridhiano ya kitaifa na kukidhi mahitaji ya wananchi. Vilevile uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Libya bado uko palepale na nchi ajinabi kama Uturuki bado zina vikosi vya jeshi katika ardhi ya Libya.

Hatua ya Bunge la Libya ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na serikali ya mpito imezusha hitilafu kubwa nchini humo na inaonekana kwenda kinyume na mwenendo uliokuwepo wa maridhiano ya kitaifa. Wakati huo huo serikali ya Libya imetangaza kuwa itaendelea kutekeleza majukumu yake hadi wakati wa uchaguzi mkuu. Misimamo hii imezusha wasiwasi mkubwa.

Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Ján Kubiš amesema: Ilitarajiwa kuwa, Bunge la Libya lingejikita zaidi katika kukamilisha sharia ya uchaguzi na kuchukua hatu zaidi za kupatikana mwafaka mpana..”

Ján Kubiš

Kwa vyovyote vile inaonekana kuwa, kuendelea mivutano ya sasa baina ya Serikali ya mpito ya Libya na Bunge yumkini kukavuruga mafanikio yaliyopatikana kuhusu jinsi ya kuitisha uchaguzi na kukomesha mgogoro wa ndani; suala ambalo bila shaka linayafurahisha madola ya kigeni na vibara wao waliozoea kuvua samaki katika maji machafu.   

Tags