Sep 24, 2021 03:06 UTC
  • Kambi ya upinzani Namibia yakataa fidia ndogo iliyotolewa na Ujerumani kwa ajili ya mauaji ya kimbari

Kambi ya upinzani nchini Namibia imewasilisha malalamiko yake dhidi ya makubaliano ya serikali ya nchi hiyo na Ujerumani kwa ajili ya kulipa fidia ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na wakoloni wa Kijerumani dhidi ya watu wa Namibia. Kambi hiyo ya upinzani ya Namibia imetoa wito wa kufanyika tena mazungumzo kuhusu suala hilo la fidia.

Wabunge wa kambi ya upinzani nchini Namibia wamekosoa makubaliano ya serikali ya nchi hiyo na Ujerumani kuhusu suala la kulipa fidia ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Wajerumani nchini humo karne moja iliyopita na kutoa wito wa kufanyika mazungumzo mapya kuhusua kadhia hiyo. 

Mwezi Mei mwaka huu serikali ya Ujerumani ilikiri kwamba ilifanya mauaji ya kimbari wakati wa ukoloni wake nchini Namibia. Ujerumani imeahidi kutoa msaada wa Euro bilioni 1.1 na kusaidia miradi ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kama fidia ya jinai zilizofanywa na wanajeshi wa nchi hiyo huuko Namibia.

Kambi ya upinzani nchini Namibia imesema fidia hiyo ni ndogo sana ikilinganishwa na jinai kubwa zilizofanywa na Wajerumai nchini kwao. 

Wakoloni wa Ujerumani waliua kwa umati makumi ya maelfu ya watu wa makabila ya Herero na Nama kwenye mauaji ya kuangamiza kizazi yaliyotokea baina ya mwaka 1904 na 1908 ambayo wanahistoria wanayataja kuwa ni mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20. Mauaji makubwa yaliyofanywa na Wajerumani na vilevile kitendo cha wakoloni hao cha kuwafukuza wanawake na watoto wadogo na kuwapeleka maeneo ya mbali majangwani kilisababisha vifo vya maelfu ya watu wa Namibia waliopoteza maisha kutokana na kiu na njaa. Wakoloni hao wa Kijerumani pia walijenga kambi za kuwatumikisha kwa nguvu raia wa Namibia.

Wanahistoria wanasema, yalikuwa mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20

Wakati wa mapigano ya Waterberg (Battle of Waterberg) Agosti mwaka 1904, karibu watu elfu 80 wa kabila la Herero wakiwemo wanawake na watoto, walikimbia nyumba na makazi yao na kukimbizwa na wanajeshi wa Ujerumani hadi kwenye Jangwa la Kalahari. Nyaraka za historia zinaonesha kuwa, watu elfu 15 miongoni mwao tu ndio walionusurika.

Jinai hiyo ya Wajerumani ilivuruga uhusiano wa Namibia na Ujerumani kwa miaka mingi. 

Tags