Sep 24, 2021 12:11 UTC
  • Nigeria yawatia mbaroni wanachama wa genge la utekaji nyara

Watu watatu wanaoshukiwa kuwateka nyara wanafunzi zaidi ya 100 katika skuli moja ya Kikristo kaskazini magharibi mwa Nigeriai miezi miwili iliyopita wametiwa mbatroni. Hayo yameelezwa na polisi ya nchi hiyo.

Tarehe 7 Julai mwaka huu watu wenye silaha walivamia shule ya sekondari ya Bethel Baptist jimboni Kaduna na kuwateka nyara wanafunzi 121 waliokuwa wamelala katika vyumba vyao. Frank Mba Msemaji wa polisi ya Nigeria ameeleza kuwa, washukiwa watatu wakuu walioshiriki katika utekaji nyara katika shule hilo wamekamatwa.

Mba ameongeza kuwa, mshukiwa mmoja kati ya hao waliokamatwa alisimamia suala la kuichunguza shule hilo ya sekondari ambaye baadaye aliwasiliana na wahalifu wenzake kabla ya kuishambulia shule na kuwateka nyara wanafunzi. Bunduki aina ya AK47 zimepatikana katika nyumba za washukiwa hao watatu na kwamba uchunguzi bado unaendelea. 

Tangu Julai 5 mwaka huu wanafunzi wamekuwa wakiachiwa huru au kufanikiwa kutoroka mikononi mwa watekaji nyara; huku taarifa zikisema kuwa wanafunzi 21 hadi sasa bado wanashikiliwa. Utekaji nyara huo wa umati umetajwa kuwa sehemu ya vitendo mtawalia vya utekaji nyara wa makundi ya uhalifu ambavyo vimeshuhudiwa kwa miezi kadhaa sasa huko kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria.

Wanafunzi wa kike wa Chibok waliotekwa nyara na Boko Haram miaka kadhaa iliyopita