Sep 25, 2021 02:34 UTC
  • Misri yaitaka Israel ijiunge na mkataba wa kupiga marufuku silaha za nyuklia wa NPT

Misri imeutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ujiunge na Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Atomiki NPT na uheshimu sheria za kimataifa.

Shirika la habari la Tasnim limemnukuu Mohammed al Mulla, mwakilishi wa Misri katika Taasisi za Kimataifa mjini Vienna, Austria akisisitiza hayo; na sambamba na kutaka eneo la Asia Magharibi lisiwe na silaha yoyote ya nyuklia amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel una wajibu wa kujiunga na Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Atomiki NPT na uache kufanya ukaidi wa kupinga matakwa ya jamii ya kimataifa katika suala hilo.

Mohammed al Mulla ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni unapaswa uruhusu wakaguzi wa kimataifa wakague taasisi zake za silaha za nyuklia na uache vitendo vyake vya kuzusha migogoro, kuvamia ardhi na maeneo ya watu wengine na kuzalisha silaha hatari za mauaji ya umati za nyuklia. 

Kiwanda chakavu cha nyuklia cha Dimona cha utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Kabla ya hapo, Balozi Hasan Khaddour, mwakilishi wa Syria katika Taasisi za Kimataifa mjini Vienna alisema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ni tishio kubwa la usalama wa dunia nzima akisisitiza kuwa, Israel ndio utawala pekee unaomiliki silaha za atomiki katika eneo la Asia Magharibi na pamoja na hayo unaendelea kukaidi kujiunga na mkataba wa NPT na hauruhusu wataalamu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kukagua shughuli zake za nyuklia.

Ripoti zinaonesha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unamiliki karibu vichwa 300 vya silaha za maangamizi ya umati za nyuklia.

Tags