Sep 25, 2021 15:18 UTC
  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
    Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameomba ushirikiano wa Watanzania ili kuyatekeleza kwa vitendo yale aliyoahidi katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York huko Marekani.

Rais Samia ameyasema hayo leo katika hafla ya kumpokea akitokea nchini Marekani.

Amesema kuzungumza kwenye taaasisi kama ile ni jambo moja, na la pili ni utekelezaji wa yale aliyoyazungumza; hivyo amewaomba Watanzania kushirikiana naye katika kuyatimiza

Amewaomba Watanzania kuungana, kushirikiana, kufanya kazi kwa pamoja kujenga taifa ambalo kwa miaka 60 sasa limekuwa likijengwa kwa awamu na hatua mbalimbali na kuongeza kuwa, kila awamu imekuwa ikiweka matofali katika kulijenga.

Ametaja mambo yaliyojadiliwa katika mkutano huo likiwemo la kuathirika kwa uchumi kutokana na maambukizi ya Covid- 19, chanjo ya maambukizi hayo na jinsi ya kushirikiana kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa huo, suala la utawala bora na mazingira.

Amesema ameiahidi dunia na Umoja wa Mataifa kwamba Tanzania itayafanyia kazi hayo yote na kuwataka Watanzania wampe ushirkiano katika kutimiza ahadi hiyo.

Tags