Sep 25, 2021 17:14 UTC
  • Watu 10 wauawa katika mlipuko wa bomu karibu na ikulu ya Rais nchini Somalia

Kwa akali watu 10 wanaripotiwa kuuawa katika mlipuko wa bomuu jirani na ikulu ya Rais katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Duru za usalama zinaripoti kuwa, shambulio hilo la bomu la kutegwa garini limetokea katika kituo cha upekuzi katika Wilaya ya Hamarweyne upande wa kusini mwa ikulu ya Rais.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, zaidi ya watu kumi wamejeruhiwa pia katika mlipuko huo wa bomu la kutegwa garini huku magari mengine yaliyokuwa yakipita jirani na eneo la tukio yakiharibiwa vibaya.

Kundi la kigaidi la wanamgambo wa al-Shabab limetangaza kuwa, ndio lililotekeleza shambulio hilo.

Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabab limekuwa likiendesha harakati za mtutu wa bunduki kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya Somalia. 

Wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia

 

Mwaka 2011, jeshi la Somalia likisaidiwa na vikosi vya Umoja wa Afrika vinavyojulikana kama AMISOM lilifanikiwa kuwatimua wanachama wa kundi hilo la kigaidi katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.

Somalia inaendelea kuandamwa na machafuko na mauaji huku muda wa Rais Mohamed Abdullahi Farmajo ukiwa umemalizika tangu mwezi Februari mwaka huu.

Hivi majuzi Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Mohamed alisimamisha madaraka ya Waziri Mkuu, Mohammed Hussein Roble ya kuajiri na kuwafuta kazi maafisa wa serikali, suala ambalo limechochea kuni katika ugomvi na mivutano inayoendelea kushuhudiwa sasa baina ya makundi ya kisiasa nchini Somalia.

Tags