Sep 26, 2021 04:34 UTC
  • HRW yakosoa hatua za karibuni za Rais wa Tunisia

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekosoa hatua zilizochukuliwa na Rais Kais Saeid wa Tunisia.

Human Rights Watch inesema hatua zilizochukuliwa na Rais wa Tunisia ni tishio kubwa zaidi kwa haki za binadamu na demokrasia nchini humo. 

Taarifa hiyo ya shirika la kutetea haki za binadamu la HRW imetolewa baada ya Rais Kais Saeid wa Tunisia kumfuta kazi Waziri Mkuu na kulisimamisha Bunge sambamba na kustisha katiba ya nchi hiyo.

Vyama vya siasa nchini Tunisia pia vimeitaja hatua hiyo kuwa ni jitihada za kuhodhi madaraka ya nchi na kuirejesha Tunisia katika utawala wa kidikteta. 

Vyama 5 vya siasa nchini Tunisia vimetoa taarifa ya pamoja vikipinga amri ya kusitishwa Katiba na kufanyiwa mageuzi.

Katika taarifa hiyo vyama hivyo vitano vya Tunisia vimetangaza kuwa, vinapinga suala la kusitishwa Katiba au kufanyiwa marekebisho na vimemtaka Rais Kais Saeid wa nchi hiyo aheshimu majukumu yake mbele ya taifa, kutekeleza Katiba na kuheshimu kiapo alichokula kabla ya kushirika wadhifa huo.

Taarifa hiyo pia imelaani ukiukwaji wa mara kwa mara wa haki na uhuru wa kimsingi wa raia ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza na kuhukumiwa raia katika mahakama za kijeshi na imemtaja Rais Kais Saeid kuwa ndiye anayepaswa kuwajibika kuhusiana na uhalifu huo.  

Tags