Sep 26, 2021 04:34 UTC
  • Wapinzani Guinea wataka maafisa 100 wa serikali ya zamani watimuliwe

Wapinzani wa serikali nchini Guinea Conakry wamekabidhi orodha yenye majina ya maafisa 100 wa serikali iliyopinduliwa wakitaka watimuliwe na kunyang'anywa nyadhifa zote za umma.

Hatua hiyo ya kambi ya upinzani nchini Guinea imechukuliwa siku 20 baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika mapema mwezi huu.

Orodha hiyo inajumuisha majina ya maafisa wengi wa serikali iliyoondolewa madarakani ya Alpha Conde akiwemo waziri mkuu wa zamani Ibrahim Kassory Fofana, aliyekuwa waziri wa ulinzi Mohamed Diané, makamanda wa polisi na askari usalama, majaji, wendesha mashtaka na wakuu wa mikoa. 

Maafisa hao wanatuhumiwa kuwa walimruhusu Alpha Conde kutwaa madaraka ya nchi Oktoba mwaka jana. Ibrahim Diallo ambaye ni miongoni mwa viongozi wa mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Konde amesema kuwa, watu waliotiwa nguvuni watafunguliwa mashtaka. 

Pamoja na hayo mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea yameendelea kulaaniwa kieneo na kimataifa huku kukitolewa miito ya kuachiliwa huru Rais Alpha Conde anayeshikiliwa kizuizini na wanajeshi waliofanya mapinduzi.

Ujumbe wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika, ECOWAS ulioongozwa na Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara na mwenzake wa Ghana Nana Akufo-Addo, ulifanya ziara ya siku moja katika mji mkuu wa Guinea na kumtaka kiongozi wa mapinduzi hayo, Kanali Mamady Doumbouya kumwachilia huru Conde na kuitisha uchaguzi mpya katika kipindi cha miezi sita.

Ujumbe wa ECOWAS ukizungumza na viongozi wa mapinduzi ya Guinea

Hata hivyo kanali Doumbouya amekataa wito huo na kuwaambia wawakilishi wa ECOWAS kuwa, kuachiliwa huru Conde ni kinyume na matakwa ya wananchi.

Doumbouya amewaambia wajumbe hao kwamba "ni muhimu kwa ECOWAS kusikiliza matakwa halali ya watu wa Guinea."