Sep 26, 2021 04:35 UTC
  • Rais Kagame: Wanajeshi wa Rwanda hawawezi kubakia milele nchini Msumbiji

Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema kuwa, wanajeshi wa nchi yake hawawezi kubakia milele katika jimbo la Msumbiji la Cabo Delgado.

Wanajeshi hao wa Rwanda wamekuwa wakishirikiana na wenzao wa Msumbiji tangu mwezi Julai, kwa ajili ya kurejesha udhibiti wa maeneo yaliyotwaliwa na wanamgambo wanaobeba silaha wenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh.

Rais Kagame ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi huko Pemba, makao makuu ya jimbo la Cabo Delgado.

Awali ujumbe huo wa wanajeshi wa Rwanda uliowasili Julai ulikuwa na azma ya kubakia kwa miezi mitatu, lakini siku ya Ijumaa Rais Kagame alisema ni jukumu la Msumbiji kuamua ni kwa muda gani wanawahitaji wanajeshi hao kubakia nchini humo. Aidha Rais wa Rwanda ametoa wito kwa nchi nyingine kuisadia Msumbiji ili iweze kukabiliana na wanamgambo hao ambao wamehatarisha amani na usalama nchini humo.

Marais wa Rwanda na Msumbiji wakiwa katika mazungumzo

 

Hatua ya askari hao wa Rwanda kutumwa Cabo Delgado inafuatia mapatano ya pande mbili wakati wa ziara ya Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi nchini Rwanda mnamo Aprili mwaka huu.

Machi mwaka huu, magaidi nchini Msumbiji waliuteka mji wa Palma wa kaskazini mwa nchi hiyo ulioko katika mpaka wa nchi hiyo na Tanzania, na kuua makumi ya watu na kuwalazimisha kuwa wakimbizi watu wengine zaidi ya 50,000. Eneo hilo limekumbwa na uasi baada ya kuanza mradi wa gesi wa dola bilioni 20.